Lugha Nyingine
Mfumuko wa bei wa Eneo la Euro wafikia rekodi mpya ya asilimia 9.1 huku kukiwa na bei za juu za nishati na vyakula (3)
Mwanamke akinunua matunda kwenye soko mjini Madrid, Hispania, Agosti 12, 2022. (Picha na Gustavo Valiente/Xinhua) |
BRUSSELS – Kwa mujibu wa makadirio yaliyochapishwa Jumatano na Eurostat, mfumuko wa bei katika eneo linalotumia sarafu ya Euro, Eurozone, ulifikia rekodi mpya ya asilimia 9.1 Mwezi Agosti huku bei za nishati na vyakula zikiendelea kupanda juu.
Mfumuko wa bei kwa Mwezi Julai ulikuwa wastani wa asilimia 8.9 katika eneo hilo lenye nchi 19.
Eurostat inakadiria kuwa nchi za Baltic zitarekodi viwango vya juu zaidi vya mfumuko wa bei kwa Mwezi Agosti, ambapo Estonia itakuwa na asilimia 25.2, Lithuania asilimia 21.1 na Latvia asilimia 20.8.
Bei ya nishati bado ndiyo kichocheo kikuu cha kuongezeka kwa mfumuko huu wa bei, huku mfumuko wa bei ukitarajiwa kufikia asilimia 38.9 mwaka hadi mwaka katika kipindi cha Mwezi Agosti. Bei za vyakula, pombe na tumbaku zinaendelea kupanda, huku mfumuko wa bei kwa mwaka huu ukitarajiwa kuwa asilimia 10.6.
Mfumuko wa bei wa mwaka baada ya mwaka kwa bidhaa zisizo za viwandani unakadiriwa pia kupanda kutoka asilimia 4.5 mwezi uliopita hadi asilimia 5 Mwezi Agosti, jambo linalowatia wasiwasi wataalamu.
"Wasiwasi mkubwa ni kuongezeka kwa kasi kwa mfumuko wa bei za bidhaa," anasema Bert Colijn, mchumi mkuu wa ING wa Eneo la Euro. "Ongezeko kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 5 limekuwa kubwa zaidi kuliko ilivyotarajiwa na kuongeza wasiwasi kuhusu madhara ya awamu ya pili kutokana na mshtuko wa gharama za uzalishaji kudumu kwa muda mrefu."
Kwa mujibu wa Eurostat, bei za huduma pia zinakadiriwa kurekodi ongezeko kidogo kutoka asilimia 3.7 Mwezi Julai hadi asilimia 3.8 Mwezi Agosti.
“Matatizo mahususi ya Ulaya yanaendelea kusukuma mfumuko wa bei kuwa juu zaidi. Mgogoro wa usambazaji wa gesi na ukame unaongeza shinikizo lililopo la upande wa usambazaji juu ya mfumuko wa bei kwa sasa,” anasema Colijn.
Mahitaji ya chini ya bidhaa ni sababu nyingine. "Pengo la pato bado ni kubwa, manunuzi ya bidhaa kwa kaya yako chini ya viwango vya kabla ya janga la UVIKO na mauzo ya rejareja kwa kweli yamekuwa katika hali ya kupungua tangu Novemba," Colijn amesema, na kuongeza kuwa eneo la euro linakabiliwa na msongamano mkubwa wa kipato halisi cha watu.
Kupanda kwa mfumuko wa bei kunaongeza shinikizo kwa Benki Kuu ya Ulaya (ECB), ambayo iliinua viwango vya riba kwa pointi 50 za msingi Mwezi Julai na inatarajiwa kuongeza viwango tena katika mkutano wake wa Septemba.
ECB inapanga kurejesha lengo lake la asilimia mbili ya kiwango cha mfumuko wa bei kwa kutumia "mbinu ya mkutano baada ya mkutano ili kuweka viwango vya riba," Philip R. Lane, mjumbe mtendaji wa Bodi ya ECB alisema Jumatatu wiki hii.
"Lengo letu kuu ni kuhakikisha kuwa sera za kifedha zinaufanya mfumuko wa bei kurejea kwa wakati kwenye lengo letu la muda wa kati la asilimia mbili," alisema Lane.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma