Lugha Nyingine
Rais wa Uganda azindua mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kwa maji uliojengwa na China (3)
Rais Yoweri Museveni wa Uganda (mwenye nguo nyeupe) akipewa maelezo wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha umeme wa megawati 600 kwa Maji cha Karuma kilichojengwa na China huko Kiryandongo, Uganda, Septemba 26, 2024. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua) |
KARUMA, Uganda - Rais Yoweri Museveni wa Uganda amezindua kituo cha kuzalisha umeme wa megawati 600 kwa maji cha Karuma na mradi wa kuunganisha umeme wa Karuma katika wilaya ya Kiryandongo ya kati-magharibi mwa Uganda. Hafla maalum ya uzinduzi imefanyika siku ya Alhamisi wiki hii na kuhudhuriwa na Makamu Rais wa Uganda, Jessica Alupo, mawaziri, maafisa waandamizi, na washirika wa maendeleo miongoni mwa wengine.
Museveni ameishukuru China kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo wa kuzalisha umeme kwa nishati ya maji, akibainisha kuwa upatikanaji wa umeme wa kutosha na wa bei nafuu ni moja ya mambo muhimu yanayoweza kuharakisha maendeleo ya uchumi wa nchi yake.
"Ninashukuru sana marafiki zetu wa China walikuja, walisema si tu tunaweza kufanya kiufundi (ujenzi), lakini pia tunaweza kutoa fedha kwa pamoja. Hivyo ndivyo tumeweza kujenga kituo hiki," rais huyo amesema.
Rais Museveni ameipongeza China kwa kutangaza kwenye Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Mwaka 2024 uliofanyika Beijing mapema mwezi huu, kwamba imesamehe ushuru kwa asilimia 100 ya bidhaa za nchi zilizoko nyuma kimaendeleo ambazo zina uhusiano wa kidiplomasia nayo, zikiwemo nchi 33 za Afrika.
Rais Museveni amesema China kwa kufungua soko lake itanufaisha nchi za Afrika.
Mradi huo wa kuzalisha umeme kwa maji, uliojengwa juu ya ardhi na chini ya ardhi kwenye Mto Nile, mto mrefu zaidi duniani, umefadhiliwa kwa pamoja na Benki ya Uagizaji na Uuzaji Nje Bidhaa ya China (EXIM) na serikali ya Uganda. Mradi huo ambao ni mkubwa zaidi nchini Uganda, umegharimu dola za kimarekani bilioni 1.7.
Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong amesema kuzinduliwa kwa mradi huo ni hatua muhimu katika ushirikiano kati ya China na Uganda.
"Mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya maji wa Karuma si tu utatoa umeme wa bei nafuu kwa mamilioni ya kaya, kusambaza umeme kwa baadhi ya maeneo ya viwanda yenye ustawi zaidi nchini Uganda, na kuendeleza mageuzi yake ya miundo ya uchumi kuwa ya kijani, bali pia utaipa nchi hiyo nguvu kubwa ya kuwa kituo cha umeme cha kikanda na kutoa mchango katika nishati safi endelevu kwa maendeleo ya Afrika Mashariki," amesema Zhang.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma