Lugha Nyingine
Watu kutoka sekta mbalimbali nchini Vietnam watoa heshima za mwisho kwa kiongozi mkuu, marehemu Nguyen Phu Trong
HANOI – Hafla ya kutoa heshima za mwisho kwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha Vietnam (CPV) marehemu Nguyen Phu Trong aliyefariki hivi karibui imeanza siku ya Alhamisi katika mji mkuu wa Vietnam, Hanoi ambapo hafla ya kushusha bendera ya taifa nusu mlingoti ilifanyika saa 12:00 jioni kwa saa za Hanoi (2300 GMT siku ya Jumatano) kwenye uwanja wa Da Dinh.
Nchi nzima ya Vietnam itakuwa na kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa siku mbili za Alhamisi na leo Ijumaa. Mashirika yote ya serikali na maeneo ya umma yatakuwa yakipeperusha bendera ya taifa nusu mlingoti, na wakaazi pia watakuwa wakionesha bendera ya taifa kutoa heshima zao. Bendera hizo zote zitakuwa zimefungwa riboni nyeusi.
Shughuli hiyo ya kutoa heshima za mwisho ilianza saa 1:00 asubuhi (00:00 GMT) kwa saa za Hanoi kwenye Ukumbi wa Mazishi ya Kitaifa mjini Hanoi, ambapo jeneza lenye mwili wa Nguyen Phu Trong, lililofunikwa kwa bendera ya taifa ya Vietnam, limewekwa.
Rais wa Vietnam To Lam, Waziri Mkuu Pham Minh Chinh, Mwenyekiti wa Bunge la Taifa, Tran Thanh Man, na Rais wa Kamati Kuu ya chama cha Fatherland Front cha Vietnam, Do Van Chien walishiriki shughuli hiyo.
Watu walikuwa wamepanga foleni katika mitaa inayozunguka ukumbi huo kutoa heshima zao za mwisho kwa mkuu huyo wa chama aliyeaga dunia.
shughuli ya kutoa heshima za mwisho pia inafanyika katika Mji wa Ho Chi Minh na katika sehemu alikozaliwa Nguyen Phu Trong kwenye jumuiya ya makazi ya Dong Hoi, eneo la Dong Anh, Mji wa Hanoi, na itaendelea hadi leo Ijumaa, ikifuatiwa na ibada ya kumbukumbu na mazishi ya marehemu.
Nguyen Phu Trong alifariki dunia Julai 19 baada ya kuugua kwa muda fulani akiwa na umri wa miaka 80, kwa mujibu wa bodi ya ulinzi wa afya na huduma wa maofisa wa serikali kuu ya Vietnam.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma