Lugha Nyingine
Okestra kutoka China yatumbuiza katika chuo kikuu cha Nairobi (5)
Wasanii wa okestra ya ala za jadi ya Chuo Kikuu cha Nanjing cha China wakitumbuiza katika Chuo Kikuu cha Nairobi jijini Nairobi, Kenya, Aprili 18, 2024. (Xinhua/Han Xu) |
NAIROBI – Okestra ya ala za jadi ya Chuo Kikuu cha Nanjing, Mashariki mwa China Alhamisi imetoa burudani ya kusisimua katika Chuo Kikuu cha Nairobi, ambacho ni chuo kikuu kikongwe zaidi nchini Kenya, na kupata makofi ya pongezi na sifa tele kutoka kwa wanafunzi na wafanyakazi wa chuo hicho waliokuwa wamekusanyika ukumbini.
Likiwa na wasanii waliokuwa wamevalia mavazi ya kuvutia, okestra hiyo ya wanafunzi imeonyesha ustadi wao katika kupiga ala za muziki za jadi za China, ikiwa ni pamoja na filimbi na ngoma.
Maonyesho hayo ya ala za muziki za jadi za China yenye jina la "China na Afrika: Uanuai, Uzuri na Mapatano", yameandaliwa na Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Nairobi kuelekea Siku ya Umoja wa Mataifa ya Lugha ya Kichina ambayo itaadhimishwa Aprili 20. Limekuwa ni sehemu ya maadhimisho hayo nchini Kenya.
Stephen Kiama, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi, amepongeza burudani hiyo ya kuvutia na kusisimua, akisema imeingiza uhai katika uhusiano wa kitamaduni kati ya China na Kenya.
"Kupitia maonyesho hayo ya Chuo Kikuu cha Nanjing, tumevutiwa na lugha na utamaduni wa Kichina ambavyo vimefungamana," Kiama amesema.
Likiwa na wasanii ambao wamechukuliwa kutoka vitivo mbalimbali katika Chuo Kikuu cha Nanjing, okestra hiyo imetoa burudani mbalimbali kama zile za nyimbo za “Kusherehekea Maua ya Jasmine”, “Safari ya Majira ya Mchipuko kwenye Mto Xiangjiang”, na “Afrika yenye Haiba”.
Maonyesho hayo yalipokamilika, kwaya kutoka Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Nairobi iliimba wimbo maarufu wa "Jambo," ambalo ni neno la Kiswahili la salamu za ukarimu, huku kukiwa na shangwe na furaha kutoka kwa watazamaji.
Edith Okinyi, mwanafunzi anayesoma masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, hakuweza kuficha furaha yake baada ya kutazama burudani yote ya ala za muziki za jadi za Kichina.
"Maonyesho hayo ya Chuo Kikuu cha Nanjing yalikuwa ya maajabu, na jinsi walivyotumbuiza kwa ala hizo ilikuwa ya kipekee. Nimependa jinsi walivyojibeba na jinsi muziki ulivyotiririka kwa kufuata midundo," Okinyi amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma