Lugha Nyingine
China yaweka mikakati zaidi kusaidia biashara za watu walioanzisha shughuli zao wenyewe
Mmiliki wa kibanda akipanga mboga katika soko la Nanning, mji mkuu wa Mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi nchini China, Julai 9, 2022. (Xinhua/Lu Boan)
BEIJING, - Maofisa wa Serikali ya China Jumanne wameahidi kuongeza juhudi zaidi kusaidia wafanyabiashara walioanzisha shughuli zao wenyewe katikati ya uwepo wa matatizo wakati nchi ya China yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani ikitangaza kanuni mpya za kuendeleza maendeleo ya biashara za watu hao.
Guo Qimin, ofisa wa Kamati ya Taifa ya Maendeleo na Mageuzi ya Kina, amesema mengi zaidi yatafanywa ili kuimarisha utekelezaji wa sera kuu, kuboresha mazingira ya biashara, na kukuza ajira na ujasiriamali.
Juhudi pia zitafanywa ili kupunguza mizigo kwa makampuni madogo na biashara za watu walioanzisha shighuli zao wenyewe, kuwasaidia kukusanya mitaji, na kuchochea mahitaji ya wanunuzi, Guo ameuambia mkutano na waandishi wa habari juu ya kanuni hizo mpya.
Kanuni hizo, zilizoanza kutumika Jumanne wiki hii, zimeweka sera maalum za upendeleo katika maeneo ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kulinda haki na maslahi halali ya biashara za kujiajiri.
Pu Chun, naibu mkuu wa Idara ya Serikali ya Udhibiti wa Soko, amesema kanuni hizo zimezingatia kikamilifu maslahi ya wafanyabiashara walioanzisha shughuli zao wenyewe na kuweka mbele hatua za kivitendo na madhubuti.
Kwa mfano, amesema, serikali za mitaa zinapaswa, kwa mujibu wa kanuni mpya, kutoa maeneo zaidi ya biashara huku zikipunguza gharama za kutumia maeneo hayo. Pia zinapaswa kuzingatia kikamilifu mahitaji na ugumu wa biashara za watu walioanzisha shughuli zao wenyewe katika kufanya maamuzi.
"Kuendeleza maendeleo ya biashara za watu hao ni kusaidia uchumi halisi," amesema Pu.
Ili kukabiliana na athari za janga la UVIKO-19 na matatizo mengine, China imefanya jitihada za mara kwa mara kupunguza mizigo kwa biashara za kujiajiri. Kuanzia Mwaka 2020 hadi mwisho wa Septemba mwaka huu, punguzo la ushuru na ada kwa biashara za watu walioanzisha shughuli zao wenyewe lilifikia karibu yuan trilioni 1.03 (kama dola za Kimarekani bilioni 142.9).
Hivi sasa, zaidi ya asilimia 80 ya biashara za watu hao nchini China hazilipishwi kodi, kwa mujibu wa Dai Shiyou, afisa wa Idara ya Ushuru ya Serikali ya China.
Takwimu rasmi zinaonesha kwamba, kufikia mwisho wa Septemba mwaka huu, China ilikuwa na biashara milioni 111 zilizosajiliwa za kujiajiri, zikichukua theluthi mbili ya wadau wote wa soko wa nchi hiyo. Takriban asilimia 90 ya biashara hizi ziko katika sekta ya huduma, wakati zaidi ya asilimia 30 zinajihusisha na biashara mpya kama vile utiririshaji wa mubashara wa maudhui mtandaoni na biashara ya mtandaoni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma