Lugha Nyingine
Maonyesho ya Tano ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) yavutia nchi, kanda na mashirika 145
Eneo la maonyesho likionekana katika picha iliyopigwa kwenye Kituo cha Taifa cha Maonesho na Mikutano cha Shanghai, eneo kuu ambalo Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) yatafanyika kuanzia Novemba 5 hadi 10 huko Shanghai, Mashariki mwa China. (Xinhua/Wang Xiang)
SHANGHAI, - Makampuni kutoka jumla ya nchi, kanda na mashirika ya kimataifa 145, yatashiriki katika Maonesho ya Tano ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China yatakayofunguliwa mjini Shanghai, China baadaye wiki hii, mratibu amesema Jumanne.
Sun Chenghai, Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya maonesho hayo, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba makampuni 284 yanayoongoza katika sekta hiyo, yakiwemo baadhi ya makampuni 500 bora duniani, yatashiriki katika maonyesho ya mwaka huu.
Maeneo mapya ya maonyesho yatafunguliwa mwaka huu yakijumuisha nyanja za mbegu za mazao na za akili bandia, wakati mamia ya bidhaa mpya za wanunuzi, kilimo, teknolojia na huduma zitaonyeshwa kwa mara ya kwanza katika maonesho hayo ya tano.
Kwa mujibu wa Sun, Ripoti ya Dunia ya Uwazi ya Mwaka 2022 itatolewa katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la Hongqiao, tukio la pembezoni mwa maonesho hayo. Jukwaa hilo la mwaka huu litafanya zaidi ya majukwaa madogo ya mijadala 20.
Maonesho ya tano ya kimataifa ya uingizaji bidhaa yatafanyika Shanghai kuanzia Novemba 5 hadi 10. Yakiwa ni maonyesho ya kwanza duniani ya uagizaji bidhaa ya ngazi ya kitaifa, Maonesho hayo yamekuwa yakifanyika katika mji mkubwa wa Shanghai, Mashariki mwa China kila mwaka tangu Mwaka 2018.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma