Lugha Nyingine
WTO yasema ukuaji wa biashara duniani utapungua sana Mwaka 2023
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) Ngozi Okonjo-Iweala (L) akizungumza kwenye Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa WTO (MC12) huko Geneva, Uswisi, Juni 15, 2022. (WTO/Kutumwa kupitia Xinhua)
GENEVA - Biashara ya Dunia inatarajiwa kupoteza kasi katika nusu ya pili ya Mwaka 2022 na kubaki katika kiwango cha chini Mwaka 2023, huku majanga mengi yakiathiri uchumi wa Dunia, Shirika la Biashara Duniani (WTO) limesema katika taarifa yake Jumatano wiki hii.
Wataalamu wa uchumi wa WTO wamesema katika taarifa hiyo kwamba kiasi cha biashara ya bidhaa duniani kitakua kwa asilimia 3.5 Mwaka 2022 – ikiwa ni bora kidogo kuliko makadirio ya asilimia 3.0 ya Mwezi Aprili. Hata hivyo, kwa Mwaka 2023 wachumi hao wanaona kutakuwa na ongezeko la asilimia 1.0, ikiwa ni chini kwa kasi kutoka kwa makadirio ya awali ya asilimia 3.4.
Makadirio mapya ya WTO yanaonesha kuwa Pato la Jumla la Dunia (GDP) katika viwango vya ubadilishaji wa soko litakua kwa asilimia 2.8 Mwaka 2022 na asilimia 2.3 Mwaka 2023 – kiwango hicho cha Mwaka 2023 ni cha chini kwa asilimia 1.0 ikilinganishwa na makadirio ya awali.
Miundombinu ya gridi ya umeme mkubwa ikionekana katika moja ya kitongoji Mjini Berlin, Ujerumani, Septemba 15, 2022. (Xinhua/Ren Pengfei)
Katika makadirio yao ya Aprili, wanauchumi wa WTO ilibidi wategemee uzoefu wa nyuma zaidi ili kutoa mwelekeo wa kuridhisha wa ukuaji wa biashara ya Dunia, kwani mgogoro wa Ukraine ndiyo kwanza tu ulikuwa umeanza na athari zake zilikuwa hazijajulikana.
Hata hivyo, wachumi wa WTO wamesema Jumatano kwamba makadirio ya Aprili kwa ajili ya biashara Mwaka 2023 sasa yanaonekana kuwa wazi kupita kiasi. Tangu wakati huo, bei ya nishati imepanda sana, mfumuko wa bei umekuwa wa msingi zaidi, na mgogoro huo bado hauonyeshi dalili ya kuisha.
Wanauchumi hao wameeleza kuwa mahitaji ya uagizaji bidhaa kutoka nje yanatarajiwa kupungua, huku ukuaji ukidorora katika nchi zenye uchumi mkubwa kwa sababu mbalimbali.
Bei ya juu ya nishati inayotokana na mgogoro kati ya Russia na Ukraine itabana matumizi ya kaya na kuongeza gharama za utengenezaji bidhaa barani Ulaya; kubana kwa sera za kifedha kutaathiri matumizi yanayozingatia maslahi katika maeneo kama vile nyumba, magari na uwekezaji usiohamishika nchini Marekani.
Kuongezeka kwa bili za kuagiza mafuta, chakula na mbolea kunaweza kusababisha uhaba wa chakula na madeni katika nchi zinazoendelea.
"Watunga sera wanakabiliwa na chaguzi zisizoweza kuepukika wanapojaribu kutafuta uwiano mzuri kati ya kukabiliana na mfumuko wa bei, kudumisha ajira kamili, na kuendeleza malengo muhimu ya kisera kama vile kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi," Mkurugenzi Mkuu wa WTO Ngozi Okonjo-Iweala amesema.
"Biashara ni chombo muhimu cha kuimarisha ugavi wa bidhaa na huduma duniani kote, na pia kupunguza gharama ya kutoa hewa chafu ya kaboni," amesema.
Picha iliyopigwa Aprili 12, 2018 ikionyesha ufupisho wa Shirika la Biashara Duniani “WTO” kwenye ukuta wa makao makuu ya Shirika la Biashara Duniani huko Geneva, Uswisi. (Xinhua/Xu Jinquan)
"Hata hivyo vizuizi vya kibiashara vinaweza kuwa jibu la kuuweka hatarini zaidi mfumo ulio dhaifu wa ugavi wa bidhaa ambao umeathiriwa na mishtuko ya miaka miwili iliyopita, kuweka vizuizi kwenye minyororo ya ugavi ya kimataifa kutaongeza shinikizo la mfumuko wa bei, na kusababisha ukuaji wa uchumi wa polepole na kupunguza viwango vya maisha kwa wakati mrefu, "amebainisha.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma