Lugha Nyingine
Takwimu zaonesha kuwa uwekezaji wa China kwenye Utafiti na Maendeleo ya teknolojia mpya (R&D) uliongezeka Mwaka 2021
Picha iliyopigwa Machi 25, 2022 ikionyesha mashine za silicon za kuzalisha karatasi ngumu za kunyonya mionzi ya jua kwenye kiwanda cha seli za jua cha silicon cha monocrystalline cha Kampuni ya PV kilichoko Mkoa wa Shaanxi nchini China. Kampuni hiyo imeongeza uwekezaji wake kwenye utafiti na maendeleo ya teknolojia mpya (R&D) ili kuboresha uzalishaji unaotumia teknolojia za akili bandia na uhifadhi wa nyenzo. (Xinhua/Shao Rui)
BEIJING - Taarifa ya kila mwaka ya takwimu za China inaonesha kuwa, kiwango cha uwekezaji kwenye utafiti na maendeleo ya teknolojia mpya (R&D) cha China, au matumizi katika R&D kwa asilimia ya pato lake la taifa, kiliongezeka hadi kufikia asilimia 2.44 Mwaka 2021.
“Kiwango hicho, kilichoongezeka kutoka asilimia 1.91 Mwaka 2012, kinaiweka China katika nafasi ya juu kati ya nchi zinazoendelea na ni cha juu kuliko wastani wa kiwango kile cha Umoja wa Ulaya,” amesema Liu Huifeng, mtafiti kutoka Taasisi Kuu ya Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ya China.
Kwa mujibu wa taarifa ya R&D ya China ya Mwaka 2021 iliyotolewa Jumatano wiki hii, Mwaka 2021, China iliwekeza yuan trilioni 2.8 (kama dola za Marekani bilioni 405) kwenye R&D, na kupanda kwa asilimia 14.6 zaidi ya ile ya Mwaka 2020. Kati ya fedha hizo, zaidi ya yuan trilioni 2, au karibu asilimia 77, zilichangiwa na makampuni.
“China inatarajiwa kutumia zaidi ya yuan trilioni 3 kwa Utafiti na Maendeleo ya teknolojia Mwaka 2022,” amesema Liu.
Liu ameongeza kuwa matumizi ya R&D ya China kutoka sekta ya biashara yalikuwa ya pili kwa ukubwa duniani mwaka jana.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa, uwekezaji wa China katika utafiti wa kimsingi katika mwaka huo ulifikia yuan bilioni 181.7, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.9 kuliko mwaka juzi. Ongezeko hilo lilichangia asilimia 6.5 ya matumizi ya jumla ya R&D, kudumisha ukuaji wa asilimia 6 na zaidi kwa miaka mitatu mfululizo.
Kwa kutazama katika mikoa nchini China, matumizi ya R&D katika mikoa ya Guangdong, Jiangsu, Beijing na Zhejiang yalikuwa katika daraja la kwanza, kwa kuzidi Yuan bilioni 200 kila mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mikoa mingi ya Katikati na Magharibi mwa China, ikiwemo Hubei, Hunan, Sichuan na Henan, ilipanda hadi kufikia Yuan bilioni 100 katika matumizi ya R&D.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma