Lugha Nyingine
INBAR yaleta ushirikiano wa China na Afrika katika matumizi endelevu ya mwanzi kwenye maonyesho ya Biashara ya Huduma (3)
Mtembeleaji wa maonyesho akipiga picha bidhaa za mwanzi kwenye banda la Shirika la Kimataifa la Mwanzi na Rattan (INBAR), Septemba 13, 2024. (Picha na People’s Daily Online) |
BEIJING - Shirika la Kimataifa la Mwanzi na Rattan (INBAR) limetumia Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Huduma ya China yanayoendelea mjini Beijing kuonyesha namna China na nchi za Kusini hasa za Afrika zinavyoshirikiana katika maendeleo endelevu ya zao la mwanzi ikichangia katika kupunguza athari za tabianchi, kupunguza umaskini na kuwezesha maendeleo ya kijani.
Akizungumza na People’s Daily Online kwenye banda la INBAR la maonyesho hayo, Mkurugenzi wa Programu za Kimataifa wa shirika hilo, Durai Jayaraman amesema China ni nchi mwenyeji wa makao makuu ya sekretatieti ya shirika hilo na imekuwa ikichangia rasilimali kama vile za kuendesha sekretarieti hiyo na katika miradi ya ushirikiano wa pande tatu na pande nyingi ambapo mbali na rasilimali, imekuwa pia ikitoa uungaji mkono wa teknolojia, ujuzi, mafunzo na ujenzi wa uwezo kwa nchi zote wanachama.
Amesema kwa sasa shirika hilo lina nchi wanachama 50, na kati ya hizo, nchi 22 ni za Afrika na kwamba kati ya ofisi tano za kikanda duniani, tatu ziko barani Afrika katika nchi za Ethiopia, Cameroon na Ghana.
Ameeleza kuwa nchi za Afrika zilizo wanachama wa shirika hilo, zimekuwa zikinufaika moja kwa moja hasa katika maeneo makuu mawili. Mosi, ni ujengaji wa mifumo ya kitaasisi ambapo shirika hilo limewezesha nchi za Ethiopia, Kenya, Uganda, Tanzania, Cameroon na Ghana kuwa na mipango mikakati na mipango kazi kuhusu uendelezaji na kutumia ipasavyo zao la mwanzi. Na pili, ni katika utendaji ambapo miradi kama vile ya ujengaji uwezo na mafunzo, utafiti wa kivitendo, upunguzaji umaskini, utoaji ajira, mabadilishano ya teknolojia na ujuzi imekuwa ikifanyika.
“Kwahiyo tunaunga mkono serikali, tunaziunga mkono nchi kwa kuzipelekea miradi, tuna miradi Afrika Mashariki, Afrika Magharibi na Afrika ya Kati” amesema Jayaraman.
Huku akibainisha kuwa mwanzi na rattan ni mazao muhimu duniani yakiwa na bidhaa zaidi ya bilioni 3 zinazouzwa kila mwaka duniani kote, Jayaraman amesema mazao hayo ni rasilimali ambazo zinapatikana kwa wingi katika nchi za Kusini yakitoa mchango mkubwa kwa ajili ya kupunguza umaskini, kupunguza athari za tabianchi, kuendeleza biashara, kutoa nafasi za ajira na kuwa mbadala wa plastiki kutokana na bidhaa zake kuwa na matumizi ya mzunguko.
Ameeleza kuwa, maonyesho hayo kama jukwaa zuri la kueneza, kuelimisha na kuonyesha watembeleaji umuhimu wa bidhaa na mazao ya mianzi lakini pia kuonesha ushirikiano wa Kusini na Kusini kupitia INBAR.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma