Lugha Nyingine
Makundi ya Palestina yatia saini Azimio la Beijing kuhusu kumaliza mgawanyiko, kuimarisha umoja wa kitaifa wa Palestina
Hafla ya kufunga mazungumzo ya maridhiano kati ya makundi ya Palestina ikifanyika Beijing, mji mkuu wa China, Julai 23, 2024. Kwa mwaliko wa upande wa China, wawakilishi wa ngazi ya juu wa makundi 14 ya Palestina walikuwa wakifanya mazungumzo ya maridhiano mjini Beijing kuanzia Julai 21 hadi 23, na makundi hayo yametia saini tamko la kumaliza mgawanyiko na kuimarisha umoja. (Xinhua/Zhai Jianlan)
BEIJING - Wawakilishi waandamizi wa makundi 14 ya Palestina walikuwa wakifanya mazungumzo mjini Beijing kuanzia Julai 21 hadi 23 ambapo Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China siku ya Jummanne alihudhuria hafla ya kufunga mazungumzo hayo na kushuhudia kutiwa saini kwa Azimio la Beijing la Kumaliza Mgawanyiko na Kuimarisha Umoja wa Kitaifa wa Palestina kati ya makundi hayo.
Wakati wa kihistoria katika mambo ya ukombozi wa Palestina
Katika hotuba yake, Wang ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), amebainisha kuwa tangu kuingia kwa zama mpya, Rais Xi Jinping wa China ametoa mapendekezo ya kutatua suala la Palestina, akitoa hekima na suluhu ya China katika kushughulikia suala hilo. Sasa, makundi 14 ya Palestina yanakusanyika mjini Beijing kwa maslahi makubwa zaidi ya taifa lao.
"Huu ni wakati muhimu wa kihistoria katika mambo ya ukombozi wa Palestina. China inapongeza juhudi za mapatano zilizofanywa na makundi yote, na kupongeza mazungumzo ya Beijing kufanyika kwa mafanikio na kutiwa saini kwa Azimio la Beijing," Wang amesema.
PLO mwakalishi pekee halali wa watu wa Palestina
Matokeo makuu ya mazungumzo kati ya makundi hayo ya Palestina yaliyofanyika Beijing ni kubainisha kwamba Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) ndicho mwakilishi pekee halali wa watu wote wa Palestina, Wang amesema.
Wang amebainisha kuwa maafikiano muhimu zaidi yaliyofikiwa katika mazungumzo haya ni kufikia mapatano makubwa na umoja kati ya makundi hayo 14, na matokeomakuu ni kuweka wazi kwamba PLO ndiye mwakilishi halali pekee wa watu wote wa Palestina.
Pendekezo la hatua tatu za kutatua suala la Palestina
Wang amesema kuwa mgogoro wa Gaza unaendelea, na athari zake zinazidi kuenea. "Ili kusaidia kuondoka katika mgogoro na hali mbaya iliyopo, China inapendekeza mpango wa hatua tatu."
Hatua ya kwanza ni kuhimiza usimamishaji vita wa pande zote, wa kudumu na endelevu katika Ukanda wa Gaza haraka iwezekanavyo, hatua ya pili ni kushikilia kanuni ya "Wapalestina kutawala Palestina" na kufanya kazi pamoja kuendeleza utawala wa baada ya vita huko Gaza na hatua ya tatu, ni kuhimiza Palestina kuwa nchi mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa na kuanza kutekeleza suluhu ya nchi mbili.
Hafla ya kufunga mazungumzo ya maridhiano kati ya makundi ya Palestina ikifanyika Beijing, mji mkuu wa China, Julai 23, 2024. Kwa mwaliko wa upande wa China, wawakilishi wa ngazi ya juu wa makundi 14 ya Palestina walikuwa wakifanya mazungumzo ya maridhiano mjini Beijing kuanzia Julai 21 hadi 23, na makundi hayo yametia saini tamko la kumaliza mgawanyiko na kuimarisha umoja. (Xinhua/Zhai Jianlan)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma