Lugha Nyingine
China kuisaidia Zimbabwe kuchimba visima kukabiliana na ukame
Visima 300 vitachimbwa katika majimbo manne ya Zimbabwe chini ya mradi unaofadhiliwa na China wa kuchimba visima uliozinduliwa jana Jumatatu katika mji wa Mahusekwa, Jimbo la Mashonaland Mashariki nchini Zimbabwe.
Mradi huo umetokana na tangazo la hali ya dharura lililotolewa na Rais wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa Machi 3 mwaka huu kutokana na ukame uliosababishwa na hali ya hewa ya El Nino unaoikabili nchi hiyo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo, Waziri wa Nyumba na Masuala ya Kijamii wa Zimbabwe, Danuel Garwe amesema, mradi huo utakuwa na athari chanya kwa maisha ya watu katika maeneo yaliyoathiriwa vibaya na ukame katika majimbo ya Mashonaland Mashariki, Manicaland, Masvingo na Midlands.
Amesema mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Geo-Engineering la China, utakuwa na msaada mkubwa katika kupunguza uhaba wa maji katika majimbo hayo manne.
Naye Balozi wa China nchini Zimbabwe Zhou Ding amesema, mradi huo ni ushuhuda mwingine wa urafiki thabiti kati ya Zimbabwe na China, na kwamba anatumai kuwa visima hivyo vitasaidia kupunguza makali ya ukame kwa Wazimbabwe.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma