Lugha Nyingine
Zimbabwe yaboresha mtandao wa barabara kabla ya mkutano wa SADC
Mfanyakazi akichapa alama za kuonesha mwelekeo wa njia kwenye barabara mpya iliyojengwa nje kidogo ya Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, Julai 20, 2024. (Picha na Tafara Mugwara/Xinhua)
HARARE - Zimbabwe inaboresha barabara ndani na karibu na mji mkuu wake Harare kabla ya Mkutano wa 44 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambao umepangwa kufanyika Agosti 17 huko Harare.
Mji huo pia unatarajia kupokea kampuni zaidi ya 150 kutoka jumuiya hiyo yenye nchi wanachama 16 wakati wa Wiki ya Maendeleo ya Viwanda ya SADC itakayofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Harare kuanzia Julai 28-Agosti 2.
SADC ina nchi wanachama za Angola, Botswana, Visiwa vya Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Ushelisheli, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Ujenzi wa barabara kuu inayoelekea kwenye jengo jipya la bunge lililojengwa na China, ambako mkutano huo utafanyika, umekamilika hivi karibuni, na usanifu na upendezaji wa mandhari ya barabara unaendelea.
Picha iliyopigwa Julai 20, 2024 ikionyesha barabara mpya iliyojengwa nje kidogo ya Harare, mji mkuu wa Zimbabwe, Julai 20, 2024. (Picha na Tafara Mugwara/Xinhua)
"Ni jambo la kufurahisha. Angalau sasa tutatumia muda mfupi wa usafiri kwenye barabara bila msungamano," Wish Gahadza, mkazi wa Harare, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua siku ya Jumamosi.
Barabara nyingine zinazoelekea kwenye jengo hilo jipya la bunge ama zimekamilika au zinaendelea kukarabatiwa.
Likiwa kwenye Mlima Hampden nje kidogo ya Harare, jengo hilo jipya la bunge lenye ghorofa sita lilikabidhiwa rasmi kwa Zimbabwe Mwezi Oktoba, Mwaka 2023.
Juhudi pia zinaendelea kukarabati barabara zinazounganisha jengo hilo jipya la bunge na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Robert Gabriel Mugabe katika mji mkuu huo wa nchi hiyo.
Aidha, serikali inaboresha mtandao wa barabara nchini humo, ikiwa ni pamoja na barabara kuu ya Harare-Chirundu inayounganisha Harare na nchi jirani ya Zambia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma