Lugha Nyingine
Biden atangaza nia ya kujiondoa kwenye uchaguzi wa urais, amwidhinisha Kamala Harris
Rais wa Marekani Joe Biden akionekana pichani katika Ikulu ya Marekani White House mjini Washington, D.C., Marekani, Julai 4, 2024, Marekani. (Xinhua/Hu Yousong)
WASHINGTON - Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza Jumapili nia yake ya kujitoa kwenye uchaguzi wa urais, baada ya idadi kubwa ya Wanachama wa chama chake cha Democrat kuelezea wasiwasi wao juu ya uwezekano wake wa kufanya kampeni na kushinda katika uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo tangu kufanya kwake vibaya kwenye mdahalo mwishoni mwa mwezi uliopita dhidi ya mpinzani wake Rais wa zamani Donald Trump.
"Ingawa imekuwa nia yangu ya kutafuta kuchaguliwa tena, naamini iko katika manufaa ya chama changu na nchi kwa mimi kukaa pembeni na kujikita zaidi kutimiza wajibu wangu wa Rais kwa muda uliobakia wa muhula wangu," Biden amesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, ambao zamani ulijulikana kwa jina la Twitter.
Amebainisha kuwa atatoa hotuba ya kitaifa baadaye wiki hii kwa undani zaidi kuhusu uamuzi wake huo.
Kwenye taarifa yake nyingine iliyochapishwa katika mtandao huo, Biden amesema anataka kutoa uungaji mkono na uidhinishaji wake kamili kwa Makamu Rais Kamala Harris kuwa mgombea mteule wa Chama cha Democrat mwaka huu. "Wanademocrat - ni wakati wa kushikamana na kumshinda Trump. Hebu tufanye hili," amesema.
Tangazo hilo la Biden, ambalo limemaliza uvumi uliodumu kwa wiki kadhaa juu ya uamuzi wake, limekuja baada ya ripoti kuibuka kuwa idadi kubwa ya Wanachama wa Chama cha Democrat wamekuwa wakimtaka ajitoe, wakiwemo watu mashuhuri kama vile Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, Spika wa zamani wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, na Kiongozi wa Wabunge Chama cha Democrat walio wengi kwenye Bunge la Seneti, Chuck Schumer.
Rais aliyeko madarakani wa Marekani na mgombea mteule mtarajiwa hajawahi kujitoa katika kinyang'anyiro cha urais katika muda kama huu wa kuchelewa kwenye mchakato wa uchaguzi hapo awali.
Kwa mujibu wa wastani wa matokeo mapya ya kura za maoni za kampuni ya Real Clear Politics, Trump anamzidi Biden katika majimbo yote muhimu ya ushindani mkali wa kura, ikiwa ni pamoja na majimbo muhimu ya Wisconsin, Michigan na Pennsylvania.
Rais wa Marekani Joe Biden na Makamu Rais Kamala Harris wakitazama fashifashi za fataki za Siku ya Uhuru zikioneshwa katika Ikulu ya Marekani White House mjini Washington, D.C., Marekani, Julai 4, 2024, Marekani. (Xinhua/Hu Yousong)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma