Lugha Nyingine
Waonyeshaji bidhaa watafuta fursa kwenye Maonyesho ya China-Eurasia (7)
URUMQI - Wafanyabiashara kutoka sehemu nyingi duniani wamekusanyika Mkoa wa Xinjiang, Kaskazini-Magharibi mwa China kwa ajili ya Maonyesho ya 8 ya China na Eurasia yanayofanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonyesho cha Xinjiang, wakionyesha bidhaa bora za kupendeza kama vile divai ya Ufaransa, kahawa ya Serbia, Chokoleti ya Australia na ngoma za Ghana.
Yakiwa na kaulimbiu ya "Fursa Mpya za Njia ya Hariri, Nguvu Mpya kwa Ushirikiano wa Eurasia," maonyesho hayo ambayo yalianza Jumatano katika mji mkuu wa mkoa huo wa Urumqi yataendelea hadi Jumapili. Yamevutia washiriki zaidi ya 1,900 kutoka nchi, maeneo na mashirika ya kimataifa 50, wakionyesha aina zaidi ya 6,000 za bidhaa.
Maonyesho hayo ambayo yamefanyika kwa mafanikio mara saba, yamekuwa njia muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Eurasia, amesema Gao Yunlong, makamu mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la Watu wa China na mwenyekiti wa Shirikisho Kuu la Viwanda na Biashara la China, kwenye hafla ya ufunguzi.
“China na nchi za Eurasia zinategemeana sana katika uchumi na zina muunganisho wa karibu katika minyororo ya viwanda na usambazaji,” amesema, huku akielezea matumaini kwa pande hizo mbili kuongeza mafungamano ya kimkakati, kuzidisha ushirikiano na kufungua ukurasa mpya katika ushirikiano wa Eurasia.
Yakichukua eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 140,000, maonyesho hayo ya mwaka huu yanajumuisha sehemu nne kuu za maonyesho zikiwemo ushirikiano wa uwekezaji, maonyesho ya kimataifa, viwanda maalum na utengenezaji wa vifaa.
Maonyesho hayo pia yameweka banda maalum kwa ajili ya Eneo la Majaribio ya Biashara Huria la China (Xinjiang) (FTZ), likilenga kuonyesha mambo ya kipekee, maendeleo na mafanikio ya maeneo matatu ya Urumqi, Kashgar na Horgos.
Tangu Mwaka 2011, awamu saba za Maonyesho ya China na Eurasia zimeshafanyika kwa mafanikio, na kutoa matokeo mazuri. Kwenye maonyesho yaliyotangulia, waonyeshaji bidhaa zaidi ya 12,200 wa ndani na nje ya China kutoka nchi na maeneo zaidi ya 70 walionyesha bidhaa, yakivutia watembeleaji jumla ya milioni 2.16.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma