Lugha Nyingine
Kenya kuwekeza dola milioni 1.9 katika kipindi cha miaka 3 ili kuboresha matumizi ya EV
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nishati la Kenya, Kenya Power, Joseph Siror akiendesha gari linalotumia umeme lililoundwa na kampuni ya JAC kutoka China jijini Nairobi, Kenya, Aprili 22, 2024. (Picha na Allan Mutiso/Xinhua)
NAIROBI - Kenya Power, ambayo ni kampuni ya usambazaji umeme nchini Kenya imesema siku ya Jumatatu kwamba itawekeza dola milioni 1.93 za Kimarekani katika miaka mitatu ijayo ili kuchochea matumizi ya magari yanayotumia umeme (EVs) nchini humo ambapo Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Joseph Siror amesema uwekezaji huo utahusu gharama ya ununuzi wa magari na pikipiki zinazotumia umeme kwa ajili ya kuunga mkono shughuli za biashara ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa vituo vya kuchajia katika maeneo mbalimbali nchini kote.
"Mbali na hitaji letu la kuchaji magari yetu yanayotumia umeme, tunakusudia kutumia vituo vyetu vya kuchaji vya EV kukusanya data ambazo zitafahamisha hatua zinazofuata katika kuunga mkono tasnia inayokua ya magari yanayotumia umeme," Siror amewaambia wanahabari mjini Nairobi.
Mnamo Septemba 2023, Kenya ilitengeneza mfumokazi wa miundombinu ya kuchaji magari yanayotumia umeme na kubadilisha betri ili kuharakisha matumizi ya EVs na kuhakikisha uanzishwaji wa huduma za kuchaji, za uhakika, zinazofikiwa kwa urahisi na za bei nafuu.
Takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli ya Kenya (EPRA) zimeonesha kuwa, EVs zilichukua asilimia 1.62 ya magari yote 165,913 yaliyosajiliwa nchini Kenya mwezi wa Desemba 2023, huku nchi hiyo ikilenga kufikia asilimia 5 ifikapo 2025.
“Mbali na vituo vya ziada vya kuchaji ambavyo tunakusudia kuvifunga katika mwaka huu wa fedha, tunalenga kufunga vituo 10 vya ziada kila mwaka katika mwaka 2025 na mwaka 2026,” Siror amesema.
EPRA imesema uwepo wa nishati mbalimbali nchini humo unafaa sana kuunga mkono vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, na asilimia karibu 85 ya uzalishaji wa nishati hutokana na nishati mbadala.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Nishati ya Kenya, Kenya Power, Joseph Siror (Kulia) akichaji gari linalotumia umeme la kampuni ya JAC kutoka China jijini Nairobi, Kenya, Aprili 22, 2024. (Picha na Allan Mutiso/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma