Lugha Nyingine
Uchumi wa kidijitali wachochea maendeleo ya kampuni za China
Mfanyakazi akionyesha seti ya kifaa cha mazoezi ya kutembea au kukimbia kinachotumia VR kwenye maonyesho yaliyofanyika wakati wa Baraza la Uchumi wa Kidijitali Mwaka 2023 katika Kituo cha Taifa cha Mikutano cha China hapa Beijing, mji mkuu wa China, Julai 4, 2023. (Xinhua/Ren Chao)
TIANJIN - Giant DC, kampuni ya teknolojia ya data iliyoanzishwa mjini Tianjin, Kaskazini mwa China miaka mitatu iliyopita, hapo awali ilikuwa kampuni inayoongoza nchini kwa kutengeneza mashine nzito ikiwa na utaalamu wa miongo kadhaa.
"Kulikuwa na uwezo wa ziada katika uzalishaji wa chuma wakati ule, na shinikizo la uhifadhi wa mazingira likiongezeka, kampuni yetu ililazimika kukumbatia mabadiliko," amesema Zhang Jian, Meneja Mkuu wa Giant DC.
Chini ya mwongozo na uungaji mkono wa serikali ya eneo hilo, kampuni hiyo ilijiondoa kwenye sekta ya chuma cha pua na chuma na kubadilika kuwa kampuni ya uchumi wa kidijitali, ikilenga ujenzi wa vituo vya data vya mtandao wa Internet na uendelezaji wa biashara kama vile uhesabu wa wingu na huduma za data.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyotolewa Mwezi Julai kwenye Baraza la Kimataifa la Uchumi wa Kidijitali Mwaka 2023 mjini Beijing, kuanzia Mwaka 2016 hadi 2022, kiwango cha uchumi wa kidijitali wa China kiliongezeka kwa dola za Marekani trilioni 4.1, ukiwa na kiwango cha ongezeko la kila mwaka la asilimia 14.2.
Kiwango cha uchumi wa kidijitali wa China kiliongezeka hadi yuan trilioni 50.2 (kama dola trilioni 6.99 za Kimarekani) Mwaka 2022, huku sehemu ya uchumi wa kidijitali katika Pato la Taifa ikipanda hadi asilimia 41.5.
Uchumi wa kidijitali umeibuka kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa China, na kampuni nyingi za kijadi nchini China, kama vile Giant DC, zimefanikiwa kutekeleza mabadiliko ya kimkakati ili kutumia uwezo wao.
Kampuni ya Vifaa vya Kielektroniki na Plastiki ya ABT (Tianjin), ambayo ni kampuni yenye ukubwa wa kati iliyoanzishwa mjini Tianjin Mwaka 2005, ilianzisha ushirikiano na Kampuni ya Huawei Cloud ambayo ni kampuni ya kutoa huduma ya wingu ili kuboresha mfumo wake uliozeeka wa kupanga rasilimali za kampuni ambao ulikuwa unatumika kwa zaidi ya muongo mmoja.
"Ushirikiano huu unaweza kutusaidia kufanikisha uzalishaji na usimamizi mtandaoni, na hata kuunganishwa na rasilimali pana za kijamii nje," amesema Shang Xiaodong, meneja mkuu wa kampuni hiyo.
"Mabadiliko ya kidijitali yanayotegemea teknolojia ya wingu yanaendelea kukua kwa kasi ya juu," Lin Zhiyong, Meneja Mkuu wa ofisi ya Kampuni ya Huawei Cloud Tawi la Tianjin amesema.
Idadi inayoongezeka ya kampuni za China zinaendeleza kwa kufuata wimbi la kidijitali. Hadi kufikia mwishoni mwa Mei, China ilikuwa imeanzisha karakana zaidi ya 1,700 za kidijitali na viwanda vya teknolojia za kisasa, ikioongoza maendeleo ya sekta hiyo. Aidha, zaidi ya majukwaa 240 ya mtandao ya viwanda yenye ushawishi wa kikanda na na katika sekta pia yameundwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma