Lugha Nyingine
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ahimiza hatua kuchukuliwa ili kukabiliana na balaa “kandamizi” la madeni
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kwenye mimbari) akizungumza kwenye mkutano wa kutolewa kwa ripoti mpya ya Kikundi cha Umoja wa Mataifa cha Kukabiliana na Msukosuko Duniani yenye kichwa "Dunia ya Madeni" kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Julai 12, 2023. Msukosuko wa madeni unaoendelea unasisitiza haja ya kuchukua hatua za dharura za kurekebisha mfumo wa mambo ya fedha duniani, Guterres amesema Jumatano. (Xinhua/Xie E)
UMOJA WA MATAIFA - Msukosuko wa madeni unaoendelea unasisitiza haja ya kuchukua hatua za dharura za kurekebisha mfumo wa mambo ya fedha duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Jumatano.
Guterres ameyasema hayo kwenye mkutano wa kutolewa kwa ripoti mpya ya Kikundi cha Umoja wa Mataifa cha Kukabiliana na Msukosuko Duniani, inayoitwa "Dunia ya Madeni."
"Nusu ya Dunia yetu inazama katika janga la maendeleo, linalochochewa na msukosuko wa madeni mazito," amesema Guterres, akinukuu ujumbe mkuu wa ripoti hiyo.
Ameongeza kuwa, watu wapatao bilioni 3.3, karibu nusu ya binadamu wote duniani, wanaishi katika nchi zinazotumia fedha zaidi kwenye malipo ya riba ya deni kuliko elimu au afya.
Akiita "kushindwa kimfumo", mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa baadhi ya nchi maskini zaidi zinalazimishwa kuchagua kati ya kulipa madeni yao au kuwahudumia watu wao.
Guterres amesema kuwa Mwaka 2022, deni la umma la kimataifa lilifikia rekodi ya dola za kimarekani trilioni 92, ambapo nchi zinazoendelea zinabeba kiasi kisicho na uwiano.
"Ni matokeo ya hali sugu ya kutokuwa na usawa katika mfumo wetu wa mambo ya fedha duniani uliopitwa na wakati, ambao unaonyesha mienendo ya nguvu ya kikoloni ya wakati ulipoanzishwa kwa mfumo huo," amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.
Amesema mfumo huo haujatimiza jukumu lake la kuwa njia salama ya kusaidia nchi zote kudhibiti majanga mfululizo ya siku hizi yasiyotarajiwa ikiwa ni pamoja na maambukizi makubwa ya UVIKO-19, athari za mabadiliko ya tabianchi na mgogoro nchini Ukraine.
Amesisitiza kuwa, mageuzi ya kina katika mfumo wa mambo ya fedha duniani hayatafanyika mara moja, lakini kuna hatua nyingi ambazo zinaweza kuchukuliwa hivi sasa.
"Hatua haitakuwa rahisi. Lakini ni muhimu, na ya dharura," Guterres amesema.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (wa kwanza kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa kutolewa kwa ripoti mpya ya Kikundi cha Umoja wa Mataifa cha Kukabiliana na Msukosuko Duniani yenye kichwa "Dunia ya Madeni" kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Julai 12, 2023. (Xinhua/Xie E)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma