Lugha Nyingine
China yapunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha utoaji wa hewa ya kaboni
Picha iliyopigwa Julai 7, 2020 ikionyesha paneli za kuzalisha umeme kwa nishati ya jua kwenye eneo maalum la viwanda katika Wilaya ya Gonghe iliyoko Eneo linalojiendesha la Hainan, Mkoa wa Qinghai, Kaskazini-Magharibi mwa China. (Xinhua/Zhang Hongxiang)
XI'AN - Ilipofika Tarehe 30 Juni, mgao wa utoaji wa hewa ya kaboni kwenye soko la kaboni la China ulikuwa tani milioni 237 ikiwa na mauzo ya zaidi ya yuan bilioni 10.91 (kama dola za Kimarekani bilioni 1.52).
“China imeanzisha soko kubwa zaidi la utoaji wa hewa ya kaboni duniani kwa ajili ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira, na imepunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha utoaji wa hewa ya kaboni,” Naibu Waziri wa Ikolojia na Mazingira wa China, Guo Fang amesema kwenye shughuli ya Siku ya Kitaifa ya China ya Utoaji Kaboni Chache siku ya Jumatano.
Shughuli hiyo imeandaliwa na Wizara ya Ikolojia na Mazingira ya China na serikali ya Mkoa wa Shaanxi, na imefanyika Xi'an, mji mkuu wa Mkoa wa Shaanxi, Kaskazini Magharibi mwa China.
Guo amesema China imepata maendeleo yenye hamasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mfululizo wa hatua kama vile kuhifadhi nishati, kupunguza kaboni, kupunguza utoaji hewa chafu, na kuanzisha na kuboresha soko la utoaji wa kaboni.
Wizara hiyo imesema, uzalishaji na uuzaji wa magari yanayotumia nishati mpya nchini China umekuwa wa kwanza duniani kwa miaka minane mfululizo, sekta yake ya nishati mbadala imeendelea kwa kasi, na mashine za kuzalisha umeme kwa upepo na jua zinashika nafasi ya kwanza duniani.
Guo amesema Wizara ya Ikolojia na Mazingira ya China itaendelea kutekeleza mkakati wa kitaifa wa kukabiliana kikamilifu na mabadiliko ya tabianchi, kuendeleza ujenzi wa soko la kitaifa la kaboni kwa hatua madhubuti na kufuata utaratibu, na kushiriki kwa juhudi zaidi katika usimamizi wa dunia inayokabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
China inalenga kufikia kilele cha utoaji wake wa hewa ya kaboni dioksidi kabla ya Mwaka 2030 na kufikia usawazishaji wa kaboni kabla ya Mwaka 2060.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma