Lugha Nyingine
Pato la Taifa la Uchumi wa Baharini wa China lazidi Yuan trilioni 9
Picha hii iliyopigwa Aprili 20, 2023 ikionyesha mandhari ya Bandari ya Guoyuan iliyoko Chongqing, Kusini Magharibi mwa China. (Xinhua/Tang Yi)
SHIJIAZHUANG – Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Uchukuzi ya China siku ya Jumanne zimeonesha kuwa, pato la taifa la uchumi wa baharini wa China, ambalo linahusisha usafirishaji baharini na uvuvi na muundaji wa meli, limezidi Yuan trilioni 9 (kama Dola za kimarekani trilioni 1.25) Mwaka 2022.
Wizara hiyo imetoa takwimu hizo kwenye jukwaa la kuadhimisha Siku ya 19 ya Bahari ya China linalofanyika katika Mji wa Cangzhou, Mkoa wa Hebei, Kaskazini mwa China, ambapo zitafanyika kwa shughuli za wiki nzima zenye mada maalumu zinazohusisha mikutano ya kitaaluma, maonyesho na shughuli za kutangaza sayansi.
Kwa mujibu wa ripoti ya wizara hiyo, takriban asilimia 95 ya bidhaa za biashara ya nje ya China husafirishwa kupitia meli za baharini.
Mwaka jana, upitishaji wa shehena za bidhaa kwenye bandari nchini China ulifikia tani bilioni 15.7, na jumla ya idadi ya makontena iliyosafirishwa ilikaribia makontena milioni 300, ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.9 na asilimia 4.7. Kiasi cha mizigo kiliongezeka kwa asilimia 33 na asilimia 56, ikilinganishwa na viwango vya miaka kumi iliyopita.
Kufikia mwisho wa Mwaka 2022, uwezo wa meli za China kubeba mizigo ulikuwa umefikia tani milioni 370 za uzito wa jumla, ikiwa ni mara mbili ya miaka kumi iliyopita, na kiwango kilipanda hadi kufikia nafasi ya pili duniani.
Siku ya Taifa ya Bahari ya China iliadhimishwa kwa mara ya kwanza Mwaka 2005 ili kuadhimisha miaka 600 ya safari za baharini za Zheng He, baharia, mgunduzi na mwanadiplomasia wa kale wa China.
Meli za mgunduzi huyo wa Enzi ya Ming (1368-1644) zilianza safari kuelekea hadi Kusini-Mashariki mwa Asia na kwingineko, na zimekuwa sehemu moja ya historia ya China ya Njia ya Hariri ya Baharini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma