Lugha Nyingine
Zaidi ya washiriki 500 kuhudhuria kongamano la sekta binafsi nchini Kenya
Zaidi ya washiriki 500 kutoka Afrika na kwingineko watahudhuria Kongamano la 14 la Umoja wa Afrika la Ngazi ya Juu la Sekta Binafsi litakalofanyika Nairobi nchini Kenya kuanzia leo Julai 10 hadi 12.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imesema kongamano hilo la siku tatu lililoandaliwa kwa pamoja na sekretarieti ya EAC na Kamati ya Umoja wa Afrika linawaleta pamoja watunga sera wa ngazi za juu za umma, watendaji wa sekta binafsi na taasisi za fedha. Washiriki wengine ni wawakilishi wa kampuni zinazomilikiwa au kuanzishwa na wanawake na vijana, wasomi na taasisi za utafiti.
Lengo la jumla la kongamano hilo lenye kauli mbiu ya "Ushirikiano wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa Ukuaji Shirikishi na Maendeleo Endelevu huku Ukiimarisha Biashara na Uwekezaji wa Kikanda na Bara kuelekea Utekelezaji wa Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA)", ni kuimarisha uhusiano kati ya masoko ya kikanda na ya bara hilo ili kuwezesha kuongezeka kwa biashara na uwekezaji. Takriban waoneshaji 100 kutoka Afrika na kwingineko wanatarajiwa kuonesha bidhaa kwenye maonyesho ya pembezoni mwa kongamano hilo yatakayofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC), mahali linapofanyika kongamano hilo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma