Lugha Nyingine
China yaongoza kwa maendeleo ya uchumi wa kidijitali duniani
Picha hii iliyopigwa Julai 4, 2023 ikionyesha gari la kuwasilisha bidhaa kiotomatiki kwa wateja likiwa kwenye maonyesho ya pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa Kidijitali Mwaka 2023 yanayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kitaifa cha China hapa Beijing, China. (Xinhua/Ren Chao) |
Beijing - China imeshuhudia ongezeko kubwa la ukubwa wa uchumi wake wa kidijitali katika kipindi cha miaka saba iliyopita, huku kukiwa na kasi ya maendeleo ya uchumi wa kidijitali duniani.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyotolewa Jumatano kwenye kongamano kuu la Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi wa Kidijitali Mwaka 2023 ulioanza Julai 4 na utafikia tamati leo mjini Beijing, kuanzia Mwaka 2016 hadi 2022, thamani ya uchumi wa kidijitali wa China iliongezeka kwa dola za Marekani trilioni 4.1, ambayo ni ongezeko la asilimia 14.2 kwa kila mwaka.
Kiasi cha uchumi wa kidijitali wa China kiliongezeka hadi yuan trilioni 50.2 (sawa na dola takribani trilioni 6.96 za Kimarekani) Mwaka 2022. Sehemu ya uchumi wa kidijitali katika Pato la Taifa la China (GDP) ilipanda hadi asilimia 41.5, na kuufanya uchumi huo kuwa injini muhimu kwa ukuaji na mageuzi thabiti.
Hivi sasa, nchi kote duniani zinaharakisha maendeleo ya maeneo muhimu ya uchumi wa kidijitali, na kuchukua kikamilifu fursa za maendeleo katika nyanja kama vile teknolojia za kidijitali na viwanda, maendeleo ya kidijitali ya viwanda na vipengele vya data.
Kwa mfano, hadi kufikia Machi 2023, waendeshaji mtandao 256 katika nchi na maeneo 95 walikuwa wameunganisha kibiashara teknolojia ya 5G, huku kukiwa na watumiaji bilioni 1.15 wa 5G duniani kote na kiwango cha asilimia 30.6 cha idadi ya watu wanaofikiwa na mtandano wa 5G, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.5 kuliko mwaka jana wakati kama huo.
Mwaka 2022, mapato yatokanayo na soko la teknolojia za akili bandia yaliongezeka hadi dola bilioni 450 za Marekani, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.3 kuliko mwaka uliopita. Idadi ya kampuni za uchumi wa kidijitali za kimataifa zenye thamani ya kuanzia dola milioni moja za Kimarekani ilifikia 1,032, ikiwakilisha asilimia 74.14 ya jumla ya kampuni hizo duniani, zikiwa na thamani inayokadiriwa ya yuan trilioni 24.95, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Mei Hong, msomi wa Akadamia ya Sayansi ya China, amesema mabadiliko ya kidijitali ya China yanasonga mbele kutoka nyanja ya matumizi na huduma hadi sekta ya viwanda katika uchumi halisi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma