Lugha Nyingine
Maonesho ya tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika kufanyika Juni 29 hadi Julai 2 huko Changsha, China
(Picha inatoka ChinaDaily)
Mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na serikali ya Mkoa wa Hunan wa China siku ya Jumanne umetangaza kuwa, Maonesho ya tatu ya Uchumi na Biashara ya China na Afrika yatafanyika kuanzia tarehe 29, Juni hadi tarehe 2, Julai katika Mji wa Changsha, Mkoa wa Hunan wa China.
Maonesho hayo yanaandaliwa kwa pamoja na Wizara ya Biashara ya China na serikali ya Mkoa wa Hunan, yakiwa na kauli mbiu ya “Kutafuta Maendeleo ya pamoja, Kunufaika na Mustakabali wa pamoja”. Nchi za Benin, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Madagascar, Malawi, Morocco, Msumbiji, Nigeria na Zambia zitakuwa nchi wageni wa heshima wa maonesho.
Kwa mujibu taarifa iliyotolewa kwenye mkutano huo na wanahabari, ukumbi mkuu wa maonesho hayo utakuwa kwenye jumba la kimataifa la mikutano na maonyesho la Changsha ukiwa na eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 100,000, ambalo ni ongezeko la karibu mita za mraba 30,000 ikilinganishwa na mwaka jana, na kutakuwa na bidhaa nyingi zaidi za kuoneshwa.
Imeelezwa kuwa, sehemu ya ukumbi, soko la Gaoqiao litakuwa ukumbi utakaotumika siku zote kwa maonesho ya ana kwa ana, likiwa na maeneo manne ya maonyesho kwa ujumla. Na katika siku hizi, tamasha la mtandaoni la kununua bidhaa bora kutoka Afrika, kuuza bidhaa mubashara mtandaoni, shindano la bingwa wa utengenezaji kahawa wa Afrika, mkutano wa kutangaza bidhaa bora za Afrika na shughuli nyingine kadha wa kadha za kuvutia zitafanyika.
Kwa mara ya kwanza maonesho haya yatatenga eneo la kuonesha mafanikio ya China na Afrika katika kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, ambalo litaonesha kutoka pande zote mafanikio mapya ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika katika zama mpya. Pia, yataweka kwa mara ya kwanza eneo la kuonesha mafanikio ya ujasirimali na uvumbuzi wa wanawake wa China na Afrika, ili kuonesha mafanikio mapya ya ushirikiano wa pande hizo mbili katika mambo ya wanawake.
Aidha, maonesho hayo yatajenga mabanda maalumu kwa nchi nane wageni wa heshima, na kusisitiza umaalumu na mitindo ya nchi hizo kupitia ubunifu wa taswira wa kila banda. Maonesho ya bidhaa na kampuni za Afrika yatakusanya bidhaa bora kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye mkutano huo, hadi kufikia tarehe 5, Juni, nchi 50 na mashirika 8 ya kimataifa yameshajisajili kushiriki kwenye maonesho hayo; Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Mkutano wa Biashara na Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCTAD), ujumbe wa Ofisi ya mambo ya Wanawake ya Umoja wa Mataifa nchini China, Shirika la Biashara la Dunia (WTO), Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Sekreterieti ya Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika na mashirika mengine ya kimataifa yatapeleka wajumbe kushiriki kwenye maonesho hayo. Inakadiriwa kuwa kwa jumla idadi ya washiriki wa maonesho hayo itazidi 10,000.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma