Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping asisitiza kujenga ustaarabu wa China wa zama za hivi sasa (2)
Rais Xi Jinping wa China, akihudhuria na kutoa hotuba muhimu kwenye mkutano wa urithi na maendeleo ya utamaduni mjini Beijing, China, Juni 2, 2023. (Xinhua/Yan Yan) |
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ametoa wito wa kubeba majukumu mapya ya utamaduni na kujenga ustaarabu wa China katika zama za hivi sasa.
Rais Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC) ameyasema hayo katika mkutano wa urithi na maendeleo ya kitamaduni uliofanyika Ijumaa.
Amesema, majukumu yetu kwenye mambo ya utamaduni katika zama mpya ni kuhimiza zaidi ustawi wa utamaduni, kujenga nchi ya China inayoongoza katika utamaduni na kuhimiza ustaarabu wa China wenye mambo ya kisasa. "Kwa kujiamini kitamaduni bila kutelekeza, kubeba majukumu makubwa na kufanya juhudi bila kulegalega, lazima tuunganishe juhudi zetu ili kuunda utamaduni mpya kwa nyakati zetu," amesema.
Rais Xi amesisitiza kuwa ustaarabu wa China una historia ndefu na endelevu inayoanzia zama za kale, na kusema kuwa uelewa mpana na wa kina wa historia hiyo ni muhimu ili kuhimiza mageuzi ya kiubunifu na maendeleo ya utamaduni mzuri wa kijadi wa China kwa ufanisi zaidi, na kuendeleza ustaarabu wa China wenye mambo ya kisasa.
Sifa maarufu za ustaarabu wa China
Rais Xi amesema, umaalum dhahiri wa ustaarabu wa China siku zote unaamua kimsingi kwamba watu wa China lazima wafuate njia yao wenyewe, na asili yake imeamua moyo wa kusonga mbele walio nao watu wa China.
“Umoja wake unaamua kimsingi kwamba tamaduni mbalimbali za makabila ya Taifa la China zimeunganishwa na kukusanyika kwa karibu, hata wakati zinakabiliwa na vikwazo vikubwa, na kwamba nchi yenye nguvu na umoja ndiyo nguzo ambayo ustawi wa watu wote wa China unategemea” ameongeza.
Kujiamini kitamaduni katika ngazi mpya
Kuunganisha kanuni za msingi za Umarx na hali halisi na utamaduni mzuri wa jadi wa China ni njia inayopaswa kufuatwa ili kuchunguza na kuendeleza ujamaa wenye umaalum wa China ndani ya ustaarabu wa China, ambao umeendelea kwa zaidi ya miaka 5,000, Rais Xi amebainisha, na kuongeza kuwa ushirikiano huu ndiyo nyenzo muhimu kwa Chama kufikia mafanikio yake.
“Licha ya asili zao tofauti za kitamaduni, Umarx na utamaduni mzuri wa jadi wa China vinaendana sana,” Rais Xi amesema.
Amesema, kuunganishwa kwa Umarx na utamaduni mzuri wa jadi wa China kutaunda aina mpya ya utamaduni unaoendana na maendeleo ya kisasa ya China, na kutapanua msingi wa utamaduni wa njia ya ujamaa wenye umaalum wa China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma