Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping afanya mazungumzo na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki
Rais Xi Jinping wa China akifanya mazungumzo na Rais Isaias Afwerki wa Nchi ya Eritrea katika Jumba la Mikutano ya Umma la Beijing, China, Mei 15, 2023. (Xinhua/Ju Peng) |
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping siku ya Jumatatu alifanya mazungumzo na Rais Isaias Afwerki wa Nchi ya Eritrea mjini Beijing.
Akipongeza urafiki wa jadi wa China na Eritrea, Rais Xi amesema nchi hizo mbili zitaadhimisha kutimia kwa miaka 30 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia Mei 24, na katika miaka 30 iliyopita, China na Eritrea zimekuwa zikiaminiana na kusaidiana.
Amesema, China inafikiria na kuendeleza uhusiano wa pande mbili na Eritrea kwa mtazamo wa kimkakati na wa muda mrefu, na China ni rafiki wa kutegemewa wa Eritrea.
Rais Xi amesema, uhusiano mzuri kati ya China na Eritrea una umuhimu mkubwa kwa amani ya kikanda na haki na usawa wa kimataifa, China inasifu Eritrea kufuata kwa muda mrefu sera yake ya mambo ya nje ya kujitawala na kujiamulia, inaunga mkono kithabiti Eritrea katika kutafuta njia ya maendeleo inayoendana na hali halisi ya nchi yake, inaunga mkono Eritrea kwa uthabiti katika kulinda mamlaka, usalama na maslahi yake ya maendeleo, na kupinga uingiliaji wa nje katika masuala ya ndani ya Eritrea na kuwekewa vikwazo vya upande mmoja.
Rais Xi amesema China iko tayari kubadilishana uzoefu na Eritrea kuhusu utawala wa nchi, kupinga kwa pamoja misimamo ya upande mmoja na umwamba, na kulinda maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili na nchi nyingine zinazoendelea.
Rais Xi amesema, haijalishi hali inaendelea vipi, kuheshimiana, kuelewana, kuungana mkono na kusaidiana siku zote zimekuwa sifa kuu za urafiki kati ya China na Afrika. Amesema ushirikiano kati ya China na Afrika unafanya kazi muhimu ya kuongoza ushirikiano wa Kusini na Kusini na ushirikiano wa kimataifa na Afrika.
"Afrika ni bara lenye matumaini. Katika mazingira mapya, ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kwa China na Afrika kuimarisha mshikamano na ushirikiano ili kukabiliana na matatizo kwa pamoja," Rais Xi amesema.
Kwa upande wake Rais Afwerki amezungumzia uhusiano wake maalum na China ambao umedumu kwa zaidi ya nusu karne, akisema kwamba watu wa Eritrea hawatasahau kamwe msaada wa thamani ambao watu wa China walitoa kwa ajili ya uhuru na ukombozi wa Eritrea.
Huku akisema jaribio lolote la kuzuia au kukandamiza maendeleo ya China halitafanikiwa, Rais Afwerki amesema kuwa China ni nchi kubwa. Tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, nchi hiyo imekua na kuwa nchi yenye nguvu duniani, ikitoa mchango mkubwa kwa amani na maendeleo ya binadamu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma