Lugha Nyingine
Mkutano wa Baraza la Boao la Asia 2023 kuhudhuriwa na watu zaidi ya 2,000
BOAO - Takriban washiriki 2,000 watahudhuria mkutano wa mwaka wa Baraza la Boao la Asia (BFA) 2023, uliopangwa kufanyika Machi 28 hadi 31 huko Boao, mji wa pwani katika Mkoa wa Hainan, Kusini mwa China, Katibu Mkuu wa baraza hilo Li Baodong amesema Jumanne.
Ikiwa ni mkutano wa kwanza wa mwaka wa nje ya mtandao wa Baraza la Boao la Asia tangu kuzuka kwa UVIKO-19, mkutano huo wa mwaka huu utahudhuriwa na watu zaidi ya 2,000 kutoka nchi na maeneo zaidi ya 50 na waandishi wa habari zaidi ya 1,100 kutoka vyombo vya habari 170 vya nchi na maeneo 40.
Mkutano huo wa mwaka huu wenye kaulimbiu isemayo "Dunia isiyo na uhakika: Kuwa na Mshikamano na Ushirikiano kwa Maendeleo kwa kukabiliana na Changamoto," utahusisha mada kuu nne, ambazo ni "Maendeleo na Jumuishi", "Ufanisi na Usalama", "Kanda na Dunia nzima", na "Hivi sasa na Siku za baadaye".
"Tunatumai kutafuta mianya ya uhakika katika Dunia isiyo na uhakika na kuhimiza mshikamano na ushirikiano kati ya nchi ili kukabiliana vyema na changamoto kupitia majadiliano kwenye mkutano wa mwaka. Pia tunalenga kudumisha uwazi na ujumuishaji ili kukuza maendeleo bora," Li amesema kwenye mkutano wa kwanza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo siku ya Jumanne.
Baraza la Boao la Asia lililoanzishwa Mwaka 2001, ni shirika lisilo la kiserikali na lisilo la faida la kimataifa linalojikita katika kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda na kuziwezesha nchi za Asia zikaribie malengo yao ya maendeleo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma