Lugha Nyingine
Thailand yakaribisha makundi ya kwanza ya watalii wa China katika kipindi cha miaka mitatu
Mtalii wa China akijipiga picha ya selfie na wafanyakazi wa Thailand katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Don Mueang huko Bangkok, Thailand, Februari 6, 2023. (Xinhua/Wang Teng) |
BANGKOK - Miaka mitatu baada ya janga la UVIKO-19, makundi ya kwanza ya watalii kutoka China yamewasili Jumatatu katika mji mkuu wa Thailand, Bangkok, yakilakiwa kwa maua na makaribisho mazuri kutoka nchi hiyo ya Kusini-Mashariki mwa Asia huku ikiweka tumaini kubwa la kufufuka kwa shughuli muhimu za utalii za nchi hiyo.
Jumatatu asubuhi, maafisa kutoka Idara ya utalii ya Thailand na Ubalozi wa China nchini Thailand walikaribisha makundi mawili ya kwanza ya watalii wapatao 20 kila moja kutoka Guangzhou kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Don Mueang. Watalii hao, ambao wako kwenye mpango wa kutalii kwa siku sita, watazuru Bangkok na kisha kuelekea eneo la kusini kwenye kituo cha mapumziko cha bahari.
Kuwasili kwa makundi haya ya watalii kunakuja wakati ambapo China, moja ya soko kubwa zaidi la utalii duniani kabla ya janga la korona , siku ya Jumatatu wiki hii imeanza tena safari za nje za makundi ya watalii.
Kuanzia Jumatatu, China imerejesha usafiri wa makundi ya watalii katika nchi 20, ikiwemo Thailand, Maldives, Falme za Kiarabu, Russia, na New Zealand.
"Thailand inaheshimika kuwa miongoni mwa nchi 20 zilizochaguliwa kukaribisha tena makundi ya watalii kutoka China. Tumefurahi sana kupokea makundi haya ya kwanza leo, na tunatarajia kuona mengine mengi yajayo," Yuthasak Supasorn, Mkuu wa Idara ya Utalii ya Thailand (TAT), amesema katika hafla ya kuwakaribisha kwenye uwanja wa ndege.
Benki Kuu ya Thailand, ilisema mwezi uliopita kwamba shughuli za utalii za Thailand zitaonyesha ufufukaji wa haraka kufuatia kurejea kwa watalii wa China, ikitarajia kwamba uchumi wa Thailand utaendelea kuimarika kwa kuendelea kufufuka kwa shughuli za utalii na matumizi katika ununuzi wa kibinafsi kutokana na kurejea kwa watalii wa China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma