Lugha Nyingine
Vitabu vya Kichina vilivyotafsiriwa vyakaribishwa kwenye maonyesho makubwa zaidi ya vitabu ya Misri
Watu wakitembelea banda la vitabu vya Kichina vilivyotafsiriwa kwenye Maonyesho ya Vitabu vya Kimataifa huko Cairo, Misri, Februari 5, 2023. (Xinhua/Ahmed Gomaa) |
CAIRO- Likiwa limepambwa kwa taa nyekundu za kijadi za China, banda la vitabu vya Kichina vilivyotafsiriwa lilishuhudia kujitokeza kwa wingi wa wapenzi wa vitabu kwenye Maonesho ya 54 ya Vitabu vya Kimataifa ya Cairo (CIBF), ambayo ni maonyesho makubwa zaidi ya vitabu katika nchi hiyo.
Banda la Bayt Al-Hekma Cultural Group, shirika la uchapishaji linalojishughulisha zaidi na tafsiri kwa Lugha ya Kiarabu ya vitabu vya Lugha ya Kichina na vile vile vitabu vya masomo ya lugha ya Kichina, limeonyesha kwenye maonyesho hayo karibu kwa vitabu 1,000 vya Kiarabu na Kiingereza kuhusu utamaduni, historia, fasihi, uchumi wa China, na mengine mbalimbali.
Watu wa rika tofauti walitembelea banda la vitabu vya Kichina kwenye maonesho hayo. Baadhi ya wazazi wa watoto walichagua vitabu vya watoto kwa ajili ya watoto wao, na baadhi ya watoto na vijana walivutiwa na vitabu vya utamaduni, historia na maendeleo ya China.
Abdel-Rahman Ibrahim, mwanafunzi wa shule ya sekondari mwenye umri wa miaka 18, ni mmoja wa vijana waliotembelea banda hilo ili kuchagua vitabu kuhusu historia ya China.
"China imeshinda matatizo mengi katika historia yake huku hekima ya Wachina ikionyeshwa katika fasihi, mawazo na falsafa," mwanafunzi huyo wa Misri ameliambia Shirika la Habari la Xinhua la China.
Maonyesho hayo pia yameshuhudia wanafunzi wengi wa Misri wanaojifunza Lugha ya Kichina wakija kwa ajili ya kujipatia vitabu, kamusi na leksimu husika ili kusaidia kuongeza ujuzi wao wa lugha.
"Nimependezwa sana na utamaduni wa China na watu wa China. Kwa hiyo, nataka kujua zaidi kuhusu China yenye ustaarabu wa kale wa lugha ya kipekee, historia, fasihi na utamaduni ," Noura Gamal, mwanafunzi wa hatua ya mwanzo wa Lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Ain Shams huko Cairo, ameliambia Xinhua.
Wakati huo huo, riwaya ya Kichina iliyotafsiriwa kwa Lugha ya Kiarabu na mtafsiri wa Misri Radwa Imbabi imeshinda tunzo ya kitabu bora cha watoto kilichotafsiriwa vizuri zaidi katika maonyesho hayo.
Ahmed al-Saeed, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya uchapishaji, amesema kuwa maendeleo makubwa ya China ni moja ya sababu za kuongezeka kwa umaarufu wa vitabu vya Kichina.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma