Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa China asema China inaunga mkono kithabiti mfumo wa biashara ya pande nyingi ambao msingi wake ni WTO
HEFEI - Waziri Mkuu wa China Li Keqiang alisema Alhamisi kwamba China inaunga mkono kithabiti mfumo wa biashara ya pande nyingi ambao msingi wake ni Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Waziri Mkuu Li ameyasema hayo wakati wa mkutano na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) Ngozi Okonjo-Iweala, ambaye alikuwa nchini China kwa ajili ya Mkutano wa Saba wa Majadiliano wa "1+6" katika Mji wa Huangshan, Mkoa wa Anhui.
Amesema, tangu kujiunga na WTO zaidi ya miongo miwili iliyopita, China kwa muda wote imetekeleza ahadi zake kwa dhati, hivyo kuchangia maendeleo yake yenyewe na kunufaisha Dunia kwa ujumla.
Waziri Mkuu Li amesema China ikiwa nchi kubwa zaidi inayoendelea duniani itashikilia kufuata kanuni ya WTO ya uwiano kati ya haki na wajibu, na kubeba majukumu yake kwa kulingana na kiwango na uwezo wa maendeleo yake ya kiuchumi.
Amesisitiza dhamira ya China ya kufanya ushirikiano na pande nyingi na kushikilia biashara huria na ya haki, na ameeleza kuwa, China ingependa kuendeleza kwa kina ushirikiano na WTO na kushirikiana na pande zote katika kuhimiza mageuzi ya WTO kwenye mwelekeo sahihi na kufikia matokeo yenye uwiano na yenye mwelekeo wa maendeleo.
Waziri Mkuu Li amesema kuwa ni muhimu matokeo ya Mkutano wa 12 wa Mawaziri wa WTO yatekelezwe kikamilifu na kwa ufanisi, ili imani ya kimataifa katika mfumo wa biashara ya pande nyingi iimarishwe.
Kwa upande wake Okonjo-Iweala amesifu sana juhudi na kazi ya kiujenzi ya China katika kudumisha mfumo wa biashara ya pande nyingi.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa WTO amesema kuwa kutengana na kukata minyororo ya ugavi siyo mwafaka kwa maendeleo ya uchumi wa Dunia na biashara ya kimataifa. WTO iko tayari kuimarisha zaidi ushirikiano na China ili kudumisha kwa pamoja mfumo ulio wazi na wenye nguvu wa biashara kati ya pande nyingi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma