Lugha Nyingine
Xi Jinping: China inaunga mkono sana mfumo wa kimataifa unaozingatia Umoja wa Mataifa
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kisiwani Bali, Indonesia, Novemba 16, 2022. (Xinhua/Yan Yan)
BALI, Indonesia - China inaunga mkono kwa dhati mfumo wa kimataifa na Umoja wa Mataifa (UN) ukiwa katika msingi wake, Rais wa China Xi Jinping amesema Jumatano alasiri alipokutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Rais Xi amesema ili kufikia amani duniani, nia na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa lazima zifuatwe, na ufuatiliaji wa nchi zote kuhusu usalama unapaswa kuzingatiwa kwa uzito.
Amesema kwamba wakati Dunia inakabiliwa na mabadiliko makubwa, ni muhimu kuweka mustakabali wa ubinadamu mbele na kufanya kazi kwa mshikamano ili kukabiliana na matatizo.
Ametoa wito kwa nchi kubwa kuwa mfano mzuri na kuchukua nafasi ya kuongoza, ili kuleta imani na nguvu zaidi kwa Dunia. Pia ameeleza imani yake kwamba amani, maendeleo na ushirikiano wa kunufaishana vinabaki kuwa mwelekeo wa kihistoria usiozuilika, na mustakabali wa binadamu utakuwa mzuri.
“Kwa sasa, mchakato wa maendeleo ya kimataifa unakabiliwa na changamoto ambazo hazijawahi kushuhudiwa na nchi zinazoendelea, hasa zile zilizo hatarini, ndizo zimeteseka zaidi,” Xi amesema.
Amesema kuwa, ni muhimu kuweka maendeleo katikati ya ajenda za kimataifa, kukuza vichochezi vipya vya maendeleo ya kimataifa, kuunda ushirikiano wa kimaendeleo wa kimataifa, kutafuta maendeleo ya kimataifa yaliyo thabiti, ya kijani na yenye uwiano zaidi, na kuruhusu kila nchi na mtu binafsi kunufaika zaidi na kwa usawa kutokana na matokeo ya maendeleo.
Amesisitiza kwamba China itaimarisha ushirikiano na Umoja wa Mataifa na kushirikiana kwa pamoja ili kupata maendeleo kwa hatua madhubuti katika Pendekezo la Maendeleo ya Dunia na Pendekezo la Usalama wa Dunia.
Kwa upande wake, Guterres kwa mara nyingine amempongeza Rais Xi kwa kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China.
Amesema kuwa nchi zinazoendelea zinakabiliwa na mfululizo wa migogoro, ikiwa ni pamoja na msukosuko wa chakula, shida ya nishati na mabadiliko ya tabianchi, huku akiongeza kuwa maendeleo ya kimataifa yanabakia kutofautiana na kutokuwa na usawa.
“Umoja wa Mataifa unapongeza dhamira ya China ya kuwa na ushirikiano wa pande nyingi, na Mpango wa Maendeleo ya Dunia ambao China imependekeza unaendana na Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu ya 2030,” Guterres amesema, na kuongeza kuwa linapokuja suala la kuzisaidia nchi zinazoendelea kupata maendeleo ya pamoja, juhudi za yeyote haziwezi kulinganishwa na juhudi za China.
Rais Xi Jinping wa China akikutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kisiwani Bali, Indonesia, Novemba 16, 2022. (Xinhua/Yan Yan)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma