Lugha Nyingine
China yashuhudia ukuaji thabiti wa biashara ya nje katika miezi 10 ya kwanza
Picha hii iliyopigwa Tarehe 11 Julai 2022 ikionyesha hafla ya kukaribisha safari ya 10,000 iliyofanywa na treni za mizigo za China-Ulaya zinazoendeshwa na Shirika la Reli la China-Ulaya (Chongqing) mjini Duisburg, Ujerumani. (Xinhua/Ren Pengfei)
BEIJING - Biashara ya China ya bidhaa ilipata upanuzi thabiti katika miezi 10 ya kwanza ya mwaka huu kutokana na sera zinazounga mkono, na mchango imara wa soko wa makampuni ya biashara na ujasiriamali.
Biashara ya nje ya China ya bidhaa iliongezeka kwa asilimia 9.5 na kufikia yuan trilioni 34.62 (kama dola trilioni 4.79 za Kimarekani) wakati wa kipindi cha kati ya Januari na Oktoba, takwimu kutoka Idara Kuu ya Forodha ya China zimeonyesha Jumatatu.
Mauzo ya nje yaliongezeka kwa asilimia 13 na kufikia yuan trilioni 19.71, wakati uagizaji wa bidhaa uliongezeka kwa asilimia 5.2 kuliko mwaka uliopita hadi kufikia yuan trilioni 14.91.
Mwezi Oktoba, biashara ya bidhaa nchini China ilifikia yuan trilioni 3.55, ikiwa ni asilimia 6.9 zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Mauzo ya nje na uagizaji kutoka nje wa bidhaa uliongezeka kwa asilimia 7 na asilimia 6.8.
Katika miezi 10 ya kwanza ya Mwaka 2022, Umoja wa Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) ulikuwa mshirika mkubwa zaidi wa biashara wa China, ambaye kiwango cha biashara yake na China kilichangia asilimia 15.2 ya jumla ya biashara ya nje.
Umoja wa Ulaya na Marekani zilikuwa washirika wa pili kwa ukubwa na wa tatu wa biashara wa China katika kipindi hicho.
Biashara ya China na nchi na kanda zinazoshiriki katika Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja imeongeza ukuaji, na mauzo ya nje na uagizaji wa bidhaa kutoka nje yameongezeka kwa zaidi ya asilimia 20.
Kwa upande wa bidhaa maalum za biashara, bidhaa za mitambo na kielektroniki, na bidhaa zinazohitaji nguvu kazi kubwa, ziliendelea kuuzwa zaidi nje, huku ya awali ikiwa ni asilimia 57.1 ya jumla ya thamani ya mauzo ya nje.
Mauzo ya magari ya China yaliongezeka kwa asilimia 72, wakati mauzo ya simu janja yaliongezeka kwa asilimia 8.7 zaidi ya mwaka uliopita.
Katika kipindi cha miezi 10 ya kwanza, uagizaji wa madini ya chuma, mafuta yasiyosafishwa, makaa ya mawe, gesi asilia na soya nchini ulipungua.
Biashara ya nje ya China imeonyesha ustahimilivu mkubwa licha ya kuzuka kwa changamoto duniani, amesema Zhou Jinzhu, mtafiti msaidizi wa Chuo cha Baraza la China la Kuhimiza Biashara ya Kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma