Lugha Nyingine
Wakulima wa parachichi wa Kenya wapata manufaa ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya China na Afrika
TIANJIN - Zola Franco, ambaye ana mkahawa wa Ki-mexico katika Manispaa ya Tianjin, Kaskazini mwa China, hivi karibuni amefanya mabadiliko mapya kwenye vyakula anavyouza.
Katika baadhi ya vyakula vinavyouzwa mahsusi kwenye mkahawa huo, amenunua parachichi za Kenya na kubadilisha zile zinazozalishwa nchini Mexico, nchi ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa parachichi duniani.
"Inapendeza sana kupika chakula cha Mexico nchini China kwa kutumia parachichi za Kenya," Franco anasema.
Wakati huo huo, takriban kilomita 8,000 katika Kaunti ya Nandi, Kaskazini-Magharibi mwa Kenya, Richard Tuwei mwenye umri wa miaka 62 tayari amevuna kundi la mwisho la parachichi. Hapo awali, sehemu nzuri ya matunda hayo ya kitropiki kutoka kwenye shamba lake la parachichi lenye takriban ekari saba (kama hekta 2.8) ilikuwa tayari imesafirishwa kupitia baharini hadi China na kuuzwa kwa bei nzuri.
Tuwei ni miongoni mwa wanufaika wa kwanza baada ya Kenya kuanza kusafirisha parachichi mbichi kwa njia ya bahari hadi China Mwezi Agosti mwaka huu, kutokana na makubaliano yaliyosainiwa na nchi hizo mbili Mwezi Januari mwaka huu.
Du Gongming, Meneja Mkuu wa kampuni ya uagizaji bidhaa kutoka Shanghai, anasema zaidi ya makontena 150 ya parachichi yanatarajiwa kuagizwa kutoka Kenya mwishoni mwa msimu wa mavuno wa mwaka huu, na takwimu hizo zinatarajiwa kufika makontena 1,500 katika msimu ujao wa Mwaka 2023.
Serikali ya Kenya inakadiria kuwa mauzo ya parachichi nchini China hatua kwa hatua yataongezeka hadi kufikia tani 100,000 kwa mwaka katika miaka michache ijayo.
Tuwei, ambaye wakati Fulani alikuwa mkulima wa mahindi, alilazimika kubadili na kuanza kulima parachichi kutokana na hasara mfululizo aliyopata iliyohusishwa na kushambuliwa na wadudu, hali mbaya ya hewa na kuyumba kwa soko.
"Nina furaha kushuhudia ufunguzi wa soko la China kwa parachichi zetu na tunatazamia kuboresha mapato kwa wakulima wa ndani ambao hapo awali walipambana na unyonyaji wa wafanyabiashara wakala ," anasema.
Ernest Muthomi, Afisa Mtendaji Mkuu katika Jumuiya ya Wazalishaji Parachichi ya Kenya, anaamini kwamba kwa vile China ni soko kubwa, makubaliano hayo mapya yataleta bahati kwa wakulima wa parachichi nchini humo.
"Usafirishaji wa parachichi kutoka Kenya kwenda nchini China unatarajiwa kuongeza mapato ya wakulima wa ndani kwa wastani wa asilimia 20 hadi 30 na kutoa makumi ya maelfu ya nafasi mpya za ajira," Du anasema.
Kuongezeka kwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika katika miongo kadhaa iliyopita kunaonekana vyema katika sekta ya parachichi.
Shukrani kwa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, Pendekezo la Ukanda Mmoja, Njia Moja na juhudi nyingine za serikali, China na Afrika zimepata ushirikiano wa kivitendo katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sekta ya kilimo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin amesema China itaunga mkono na kuwezesha kuingizwa kwa bidhaa za kilimo na chakula bora za Afrika katika soko la China, na kuleta manufaa zaidi kwa watu wa China na Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma