Lugha Nyingine
Marais wa China na Indonesia waaahidi juhudi za pamoja za kujenga jumuiya yenye mustakabali wa pamoja
Rais Xi Jinping wa China akifanya mazungumzo na Rais wa Indonesia aliyezuru China Joko Widodo kwenye Jumba la Wageni la Taifa la Diaoyutai la Beijing, Julai 26, 2022. (Xinhua/Pang Xinglei) |
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping siku ya Jumanne alifanya mazungumzo na mwenzake wa Indonesia aliyezuru mjini Beijing Joko Widodo. Marais hao wawili walikuwa na mazungumzo kwa kina na kufikia mfululizo wa makubaliano muhimu kuhusu uhusiano kati ya China na Indonesia na masuala ya kimataifa na kikanda yenye maslahi kwa pande zote.
Akielezea furaha yake kwamba pande hizo mbili zimeamua mwelekeo wa jumla wa kujenga jumuiya ya China na Indonesia yenye mustakabali wa pamoja, Xi amesema China itashirikiana na Indonesia kuimarisha hali ya kuaminiana kimkakati na kusaidiana kithabiti katika kutetea mamlaka ya nchi, usalama na maslahi ya maendeleo, katika kufanya utafiti kuhusu njia za maendeleo zenye kuendana na hali ya taifa, na katika kuhimiza uchumi na kuboresha maisha ya watu.
Uthabiti na uhai wa uhusiano wa pande mbili
Akiweka bayana kuwa Rais Widodo ni mkuu wa kwanza wa nchi kufanya ziara nchini China baada ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing, Xi alisema hii inaonesha vya kutosha kuwa pande hizo mbili zinazingatia sana kuhimiza maendeleo ya uhusiano wa nchi hizo mbili
Xi alisema uhusiano kati ya China na Indonesia umepata ukuaji mkubwa katika miaka ya hivi karibuni, na kuonyesha uthabiti na uhai mkubwa. Amesema, kuaminiana kimkakati kumeimarishwa zaidi, na ushirikiano wenye nguzo nne, yaani, ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi, kati ya watu na watu na wa kwenye bahari umeendelea kuongezeka.
"Ukweli umethibitisha kuwa uhusiano mzuri kati ya China na Indonesia siyo tu kwamba unatumikia maslahi ya pamoja ya muda mrefu ya nchi hizo mbili, lakini pia una matokeo mazuri na makubwa ya kikanda na kimataifa," Xi alisema.
Kwa upande wake, Rais Widodo alisema Indonesia na China ni wabia wa kimkakati na wa kina wenye lengo muhimu la kujenga kwa pamoja jumuiya yenye mustakabali wa pamoja, na kuongeza ushirikiano wao ni kwa manufaa ya pande zote mbili, siyo tu katika kuwahudumia vyema watu wa nchi hizo mbili bali pia kuchangia kwa kiasi kikubwa amani na maendeleo kwenye kanda na kwingineko.
Jumuiya ya China na Indonesia yenye mustakabali wa pamoja
Xi alisema kuwa China na Indonesia ziko katika hatua sawa za maendeleo, zimeunganisha maslahi, zinafuata falsafa na njia za maendeleo zinazofanana, na zina uhusiano uliounganishwa wa mustakabali wa baadaye. "Kujenga jumuiya ya China na Indonesia yenye mustakabali wa pamoja ni matamanio na matarajio ya pamoja ya watu wa pande hizi mbili," Xi amesema.
Xi pia alisema China itaendelea kuunga mkono kikamilifu Indonesia katika kujenga kituo cha kikanda cha uzalishaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19, kukamilisha reli ya treni za mwendo kasi ya Jakarta-Bandung kwa wakati uliopangwa na kwa kiwango cha juu, kuongeza ushirikiano na Indonesia kwenye afya ya umma, kuhakikisha utekelezaji wa mradi wa Ukanda wa Kiuchumi wa Kikanda na "Nchi Mbili, Maeneo Pacha Maalumu ya Kiuchumi”, kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya mji mkuu mpya wa Indonesia na Eneo Maalumu la Viwanda la Kalimantan Kaskazini.
Kusimama pamoja kwa mshikamano
Rais Xi alisema China na Indonesia zinapaswa kusimama pamoja kwa mshikamano, kutekeleza majukumu ya nchi kubwa zinazoendelea, kufuata msimamo wa pande nyingi, kushikilia msimamo wa wazi wa kikanda, kuchangia hekima ya Mashariki na mchango wa Asia kwenye maendeleo ya usimamizi wa Dunia.
Xi alisema China inaiunga mkono kikamilifu Indonesia kuwa mwenyeji wa Mkutano wa G20 huko Bali, kuunga mkono Umoja wa Nchi za Kusini-Mashariki za Asia (ASEAN) na inakaribisha kuendelea kwa Indonesia kushiriki kikamilifu kwenye ushirikiano wa "BRICS Plus".
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma