Lugha Nyingine
Makala: Bidhaa za China zavutia watembeleaji wa Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
DAR ES SALAAM - Makumi kwa mamia ya watembeleaji wa maonyesho wa ndani na nje ya Tanzania wanaotembelea Maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) wanamiminika kwenye banda la China kutafuta taarifa za bidhaa mbalimbali zinazoonyeshwa.
Vifaa vya viwandani, usindikaji na vifaa vya ujenzi kutoka China vimekuwa vikiuliziwa na watu wanaotembelea banda hilo tangu maonyesho hayo ya biashara yafunguliwe milango yake Juni 28 katika mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam, nchini Tanzania.
Banda la China linawakilishwa na Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Centre (EACLC Limited) inayohimiza biashara kati ya Tanzania na China. Cathy Wang, Mkurugenzi Mkuu wa EACLC Limited, anasema makampuni 52 kutoka Mkoa wa Shandong wa China yako katika banda hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 450.
Banda la China linaonesha bidhaa mbalimbali zikiwemo za kilimo, mashine za kilimo, nguo, vifaa vya ujenzi, bidhaa za vifungashio, vipuri vya magari, vifaa vya kielektroniki na samani, jenereta za umeme na mashine za kusindika vyakula na vifaa vya pikipiki. Bidhaa hizi zote zinazalishwa katika Mkoa wa Shandong.
Aidha, banda la China limeialika Taasisi ya Confucius kuandaa maonyesho ya kichina ya ngoma ya simba na KungFu, ambayo yanavutia watazamaji wengi.
Wang amesema ushiriki wa kampuni za Shandong umeandaliwa na Idara ya Biashara ya Mkoa wa Shandong.
“Uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na China umeimarika wakati wa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na dhamira yake ya kuhimiza uhusiano wa kimataifa,” amesema.
Kwa mujibu wake, hali ya biashara inazidi kushamiri nchini Tanzania na jumuiya ya wafanyabiashara kutoka Shandong inatafuta soko la uhakika la vifaa katika sekta ya kilimo, viwanda na ujenzi.
"Idara ya Biashara ya Shandong inafanya kazi ya kukuza wajasiriamali wa ndani ili kuchunguza kwa pamoja soko la Afrika na bidhaa halisi. Hii inakwenda sambamba na kuweka mazingira mazuri kwa makampuni ya biashara kukua na kutoa ajira, kuanzisha viwanda na uwekezaji mkubwa barani Afrika hasa Tanzania,” amesema.
Tangu lilipofunguliwa milango yake, banda hilo la China limetembelewa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Mizengo Pinda na Ashatu Kijaji, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara wa Tanzania.
Kwa mujibu wa ubalozi wa China nchini Tanzania, Mwaka 2020, thamani ya biashara kati ya China na Tanzania ilifikia dola za Marekani bilioni 4.58.
Maonyesho hayo yatakayofikia tamati Julai 13 imevutia makampuni 180 ya kigeni na makampuni 3,200 ya Tanzania yanayoonyesha bidhaa, huduma na teknolojia zinazotumika katika uzalishaji wa bidhaa.
DITF ni tukio kuu la kila mwaka la kutangaza na kuonesha bidhaa ambalo limejiimarisha kwa miaka mingi kama dirisha la duka la bidhaa za Tanzania na pia kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma