Lugha Nyingine
Nchi za Eneo la Euro zakabiliana na msukosuko wa kiuchumi kwa njia tofauti, na kuibua changamoto kwa Benki Kuu ya Ulaya
Picha iliyopigwa Juni 1, 2022 ikionyesha sanamu ya nembo ya Eneo linalotumia Sarafu ya Euro huko Frankfurt, Ujerumani. (Xinhua/Lu Yang) |
ROME – Nchi zinazotumia sarafu ya Euro, zinazowakilishwa kwa pamoja kwa jina la Eneo la Euro zinakabiliana kwa njia zilizo tofauti na mtikisiko wa kiuchumi wa wiki za hivi karibuni, na kuongeza changamoto kwa Benki Kuu ya Ulaya (ECB) inapojiandaa kuongeza viwango vya riba kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.
Kiashiria cha kiuchumi ambacho wanauchumi wengi wanakizingatia ni mfumuko wa bei. Kwa mujibu wa Eurostat, bei katika nchi 19 za Eneo la Euro ilipanda na kufikia kiwango cha juu zaidi cha asilimia 8.6 mwezi Juni ikilinganishwa na mwezi huo huo Mwaka 2021.
Idadi hiyo ilivunja rekodi ya kiwango cha juu cha mfumuko wa bei kwenye eneo la euro kilichowekwa mwezi mmoja tu uliopita, ambapo Mwezi Mei mfumuko wa bei wa mwaka hadi mwaka ulikuwa asilimia 8.1.
Viashiria vingine vilitofautiana vile vile: viwango vya ukosefu wa ajira kwenye eneo hilo katika kipindi cha hivi punde cha kuripoti vilianzia asilimia 2.8 nchini Ujerumani hadi asilimia 13.1 nchini Hispania. Makadirio ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka huu katika Eneo la Euro yalitofautiana kutoka asilimia 1.0 tu nchini Estonia hadi asilimia 5.8 nchini Ureno.
"Tatizo kubwa linalokabili uchumi wa Eneo la Euro hivi sasa ni kutokuwa na uhakika," Giuseppe De Arcangelis, profesa wa uchumi wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha La Sapienza cha Roma, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.
De Arcangelis alikuwa akizungumzia ongezeko la bei na athari nyingine zinazotokana na mgogoro wa Ukraine, pamoja na sera ya fedha kutoka Benki Kuu ya Ulaya (ECB), ambayo imesema itaongeza viwango vya riba mwezi huu kwa mara ya kwanza tangu Mwaka 2011 katika jaribio la kupunguza shinikizo la mfumuko wa bei kwa kupunguza uingizaji fedha za euro kwenye mzunguko.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, athari ya papo hapo imekuwa kuimarika kwa mahitaji ya hati fungani kutoka kwa mataifa yenye uchumi imara ya ukanda huo kama vile Ujerumani na Uholanzi, na viwango vya juu vya riba kwa nchi zenye madeni zaidi kutoka Kusini mwa Ulaya, zikiwemo Italia, Ugiriki na Hispania.
Huku nchi tofauti zikikabiliana na misukosuko ya kiuchumi kwa njia tofauti, inaongeza changamoto kwa ECB inapotafuta mkakati bora wa jumla wa kisera kwa nchi 19 za Eneo la Euro.
"Sera ya fedha iko katika wakati mgumu," Rais wa ECB Christine Lagarde amesema mapema wiki hii katika kongamano la kila mwaka la benki hiyo nchini Ureno, taarifa ambayo iliwashangaza waangalizi wachache.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma