Lugha Nyingine
Wanafunzi wa vyuo vikuu Tanzania wafanya vyema katika mashindano ya Lugha ya Kichina
DAR ES SALAAM - Wanafunzi kumi na wawili wa vyuo vikuu nchini Tanzania, ambao nyuso zao zilimelemeta kwa tabasamu pana, Ijumaa walikusanyika ili kushindana katika Mashindano ya 21 ya Ustadi wa Lugha ya Kichina ya Daraja la Kichina kwa Mwaka 2022 kwenye Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Wanafunzi hao walioshiriki mashindano hayo kupitia video zilizotayarishwa, walitoka katika Taasisi ya Confucius iliyopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dodoma na Darasa la Confucius la Chuo Kikuu cha Zanzibar.
Baada ya mchuano mkali uliochukua saa mbili, Adam Nyenje, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Lugha ya Kichina kutoka Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Dodoma alitangazwa mshindi wa jumla. Nyenje baadaye mwaka huu atasafiri hadi China kushindana katika Mashindano ya Kimataifa ya Ustadi wa Lugha ya Kichina ya Daraja la Kichina.
Malengo makuu ya mashindano hayo ni kutathmini ustadi wa wanafunzi katika ujuzi mbalimbali wa lugha ya Kichina kama vile kutoa hotuba kwa Kichina, na ujuzi kuhusu China pamoja na kuonyesha vipaji.
Makamu Mkuu wa Chuo cha UDSM, William Anangisye aliishukuru Taasisi ya Confucius iliyopo chuoni hapo kwa kuandaa mashindano hayo, na kusema kuwa tukio hilo linakuza na kuwatia moyo wanafunzi wengi wanaopenda kujifunza lugha ya Kichina na kuonyesha vipaji mbalimbali ikiwemo utamaduni wa China.
Anangisye anaamini kuwa kujifunza lugha ya Kichina ni mbinu mwafaka ya kuendeleza uhusiano kati ya China na Afrika.
Amesema kuwa UDSM inatoa Shahada ya Sanaa ya Elimu (kwa lugha za Kichina na Kiingereza) kwa wanafunzi ambao baadaye watafundisha lugha ya Kichina katika shule za msingi na sekondari Tanzania nzima.
Naye Konsela wa Utamaduni wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, Wang Siping ameishukuru Serikali ya Tanzania hususani Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Confucius ya UDSM kwa kuunga mkono ukuzaji wa lugha ya kichina na utamaduni wa China.
Wang ambaye alikabidhi vyeti kwa baadhi ya washindi, amesema Ubalozi wa China nchini Tanzania utasaidia ufundishaji wa lugha ya Kichina shuleni katika ngazi zote.
Shindano hilo pia lilishuhudiwa na Aldin Mutembei na Zhang Xiaozhen ambao ni wakurugenzi wa Taasisi ya Confucius iliyopo UDSM ambao walikabidhi vyeti kwa washindi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma