Lugha Nyingine
Coca-Cola yazindua kiwanda cha kutengeneza vinywaji baridi nchini Ethiopia chenye thamani ya dola za kimarekani milioni 100
ADDIS ABABA - Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola Afrika (CCBA) Jumanne wiki hii imezindua kiwanda chake kipya nchini Ethiopia chenye thamani ya dola milioni 100 za kimarekani.
Kampuni hiyo imesema kwamba, kukamilika kwa kiwanda hicho kutawezesha kiwango cha uzalishaji wa CCBA nchini Ethiopia kufikia chupa milioni 100 kwa mwaka na itawezesha kampuni kuunganisha uzalishaji wa pembejeo kama vile preforms, vifungashio na vifaa vingine, pamoja na uzalishaji wa ndani wa bidhaa mpya huku ikipunguza uagizaji kutoka nje.
Kiwanda hicho kipya kilichopo nje kidogo ya Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, katika Mji wa Sebeta, kimezinduliwa mbele ya maafisa wakuu wa serikali ya Ethiopia pamoja na wawakilishi kutoka kampuni hiyo.
Waziri wa Viwanda wa Ethiopia Melaku Alebel amesema kwenye hafla ya uzinduzi kwamba, kiwanda hicho kipya kinaonyesha imani ya kampuni hiyo kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki wakati wa shughuli zake za zaidi ya miongo sita nchini humo.
Waziri huyo amesisitiza zaidi kwamba Serikali ya Ethiopia kwa sasa inafanya juhudi mbalimbali ambazo zinalenga kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji waliopo na wapya katika sekta ya viwanda nchini humo.
Kampuni hiyo imesema pamoja na kukidhi mahitaji yake katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, uzalishaji wa malighafi katika kiwanda hicho kipya umepangwa kwa ajili ya soko la nje ili kuingiza fedha za kigeni na kusambazwa kwenye soko la ndani ili kusaidia kutatua uhaba wa sekta hiyo.
"CCBA inajivunia kuwa kiongozi wa sekta katika kuhimiza njia endelevu za kuzalisha, kusambaza na kuuza bidhaa zetu," Mkurugenzi Mtendaji wa CCBA, Jacques Vermeulen amesema kwenye hafla hiyo ya uzinduzi.
"Tunalenga kutengeneza fursa kubwa zaidi za pamoja kwa ajili ya biashara na jamii mwenyeji wetu katika mnyororo wa thamani."
"Kupitia uwekezaji wetu nchini Ethiopia, tumeongeza fursa za ajira za moja kwa moja kutoka 1,000 Mwaka 2012 hadi zaidi ya 3,500 Mwaka 2022, wakati zaidi ya watu 70,000 ni wanufaika wa mnyororo wetu wa thamani," ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma