Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping azungumza na Macron kwa njia ya simu
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping jana Jumanne mchana alikuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Xi aliweka bayana mawasiliano yake ya karibu na Macron katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ambayo yamesaidia kuziongoza nchi hizo mbili katika kudumisha kasi ya maendeleo ya uhusiano, kutengeneza ushirikiano wenye kuzaa matunda, na kutekeleza majukumu ya nchi kubwa juu ya mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa viumbe anuai na masuala mengine.
Xi alisema, kwa kukabiliwa na mabadiliko makubwa ambayo hayakutokea hapo kabla katika karne moja iliyopita, China na Ufaransa, zikiwa nchi mbili za wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi kubwa huru, zinapaswa kushikilia nia ya awali wakati wa kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia ya " kujitawala na kujiamulia, kuelewana, kutupia macho mbali na kufanya ushirikiano wa kunufaishana" ,kuendelea na ushirikiano wao wa kimkakati wa karibu na wa kudumu, kuheshimu masilahi ya msingi ya kila upande na mambo makuu yanayohusu kila mmoja wao, na kuimarisha uratibu na ushirikiano katika mazingira ya pande mbili, China na Umoja wa Ulaya na kwenye ngazi ya kimataifa.
Xi alizungumzia umuhimu wa nchi hizo mbili kupanua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta mbalimbali zikiwemo teknolojia za akili bandia na nishati safi, huku zikiendeleza ushirikiano katika maeneo ya jadi kama nishati ya nyuklia, sekta ya usafiri wa ndege na anga ya juu. Xi pia amekaribisha makampuni ya Ufaransa kuwekeza China na kusema kwamba China iko tayari kununua bidhaa bora kutoka Ufaransa.
Xi alisema ni muhimu China na Ufaransa kutumia vyema matukio makubwa kama vile mwaka wa 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Ufaransa na Michezo ya Olimpiki ya Paris itakayofanyika Mwaka 2024, kama fursa muhimu za kuongeza mabadilishano zaidi baina ya watu na ya kiutamaduni na kuongeza maelewano.
Aliongeza kuwa pande hizo mbili zinapaswa kufanya ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, kushikilia mfumo wa kimataifa ambao Umoja wa Mataifa ukiwa msingi wake na utaratibu wa kimataifa unaofuata sheria za kimataifa, kuunga mkono usawa wa mataifa yote duniani na utandawazi wa kiuchumi, na kuzidisha ushirikiano katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi na viumbe anuai.
Xi alisisitiza kuwa pande hizo mbili zinahitaji kuongeza mawasiliano na uratibu katika Kundi la Nchi 20 (G20) na juu ya usalama wa chakula na nishati duniani, kupanua ushirikiano wa pande tatu barani Afrika na kanda nyingine, na kushirikiana kwenye mipango ya China ya Pendekezo la Maendeleo ya Dunia Nzima na Pendekezo la Usalama wa Dunia Nzima.
Xi pia alielezea umuhumi wa uhusiano wa China na Umoja wa Ulaya katika kukuza uchumi, kuboresha maisha ya watu wa pande hizo mbili na katika ustawi kwenye sekta mbalimbali. Alielezea matumaini yake kuwa, Ufaransa ikiwa nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya, itafanya juhudi za kiujenzi katika kukuza maendeleo mazuri ya uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya.
Kwa upande wake, Macron alipongeza moyo wa wazi ambao pande hizo mbili zimeendeleza katika uhusiano wao tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia.
Alisema katika miaka mitano ijayo, Ufaransa itashirikiana na China kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali, na Ufaransa inapenda kufanya juhudi za kiujenzi za kuhimiza maendeleo ya uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya
Viongozi hao pia walizungumzia kwa kina hali ya vita nchini Ukraine ambapo walisisitiza haja ya suluhu ya amani, Ulaya kuwa na mfumo ulio wa usawa wa kiulinzi na kuepuka siasa za kijiagrafia zenye mtafaruku.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma