Lugha Nyingine
Xi atoa wito kwa juhudi za kujenga mfumo wa miundombinu ya kisasa
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping siku ya Jumanne wiki hii ametoa wito kwa juhudi za kila namna kuimarisha ujenzi wa miundombinu katika mpango wa nchi hiyo wa kujenga mfumo wa miundombinu ya kisasa.
Xi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China, aliyasema hayo kwenye mkutano wa 11 wa Kamati Kuu ya Masuala ya Fedha na Uchumi, kamati ambayo Xi Jinping ni mwenyekiti wake. Miundombinu ni nguzo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Xi amesema, huku akihimiza nchi hiyo kuratibu maendeleo na usalama, na kuboresha mpangilio, miundo, uwezo wa kazi na mfano wa maendeleo.
Viongozi wengine wa China akiwemo Li Keqiang, Wang Huning na Han Zheng wamehudhuria mkutano huo.
Mkutano huo umesikiliza na kupokea ripoti za kazi kutoka kwa idara husika juu ya kuimarisha ujenzi wa miundombinu na maendeleo yake katika utekelezaji wa sera.
Huku ukitoa pongezi kwa mafanikio ya China katika ujenzi wa majengo muhimu ya teknolojia ya sayansi, miradi ya kuhifadhi maji, mfumo wa mawasiliano , miundombinu ya upashanaji wa habari na akiba za kimkakati za taifa, mkutano huo umezingatia kuwa miundombinu ya nchi hiyo bado haiendani na mahitaji ya maendeleo na usalama wa taifa.
Kwa mujibu wa mkutano huo, kuimarisha ujenzi wa miundombinu kwa pande zote kuna umuhimu mkubwa katika kuhakikisha usalama wa taifa, kulainisha usambazaji wa bidhaa ndani ya nchi, kuhimiza "mizunguko miwili " ya soko la ndani na la nje , kupanua mahitaji ya ndani ya nchi na kukuza maendeleo ya kiwango cha juu.
“Katika kufikia lengo hili, nchi inahitaji kufanya juhudi za kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya mitandao ya mawasiliano barabarani na majini , nishati na uhifadhi wa maji, ili kuboresha ufanisi” mkutano huo umesema.
Mkutano huo umesisitiza kwamba, China inapaswa kukamilisha upangaji wa njia za maji na ujenzi wa bandari za majini na nchi kavu, na kuboresha ujenzi wa majengo ya usafirishaji wa majini kote nchini, kujenga mfumo wa gridi ya kisasa, , vituo vipya vya nishati ya kijani na vya kutoa kaboni ndogo, na mtandao wa bomba la mafuta na gesi unapaswa kupangwa vizuri.
Mkutano huo pia umesisitiza maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya teknolojia za akili bandia, mifumo ya kompyuta na intaneti, ujenzi na ukarabati wa viwanja vingi vya ndege vya mikoa, vya jumla na vya usafirishaji wa mizigo kote nchini na uboreshaji wa mitandao ya teknolojia za mawasiliano.
Mkutano huo pia umeeleza kwamba, China inahitaji kukuza kilimo cha kisasa na kustawisha maeneo ya vijijini kupitia ujenzi wa miundombinu, huku pia ukisisitiza umuhimu wa kusaidia miundombinu ya usalama wa taifa na kuongeza uwezo wa nchi katika kukabiliana na hali mbaya.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma