Lugha Nyingine
China yatia saini mikataba ya ushuru na nchi 21 za Afrika
BEIJING - China imetia saini mikataba ya ushuru na nchi 21 za Afrika hadi sasa, afisa wa Mamlaka ya Taifa ya Ushuru ya China (STA) amesema siku ya Jumatatu, akiongeza kuwa mamlaka za ushuru za China zinatafuta fursa za kuongeza ushirikiano wa kimataifa wa ushuru na nchi za Afrika.
Meng Yuying, mkuu wa Idara ya Mambo ya Ushuru ya Kimataifa ya STA, amesema hayo kwenye mkutano na waandishi wa habari wa Mkutano wa Kilele wa 2024 wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Meng amesema nchi za Afrika ambazo zimetia saini mikataba ya ushuru na China ni pamoja na zile zenye hisa kubwa ya uwekezaji wa moja kwa moja na China.
Mikataba hiyo ya ushuru inatoa msingi muhimu wa kisheria wa kimataifa kwa uwekezaji na biashara ya kuvuka mipaka, Meng amesema, akiongeza kuwa inaweza kuzuia hali ya kutozwa ushuru mara mbili kwa bidhaa au huduma moja, kutoa uhakika wa ushuru na kuwezesha utatuzi wa migogoro ya ushuru.
"Inasaidia kujenga mazingira ya ushuru na biashara ya kimataifa yaliyo ya haki, mazuri na ya kunufaishana, na kukuza uwekezaji wa kuvuka mipaka na mawasiliano ya teknolojia na wafanyakazi," amesema.
Meng amesema kuwa utaratibu wa ushirikiano wa ukusanyaji na usimamizi wa ushuru wa Ukanda Mmoja, Njia Moja ulianzishwa katika Mkutano wa pili wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Ukanda Mmoja, Njia Moja Mwaka 2019, na kwamba nchi nyingi za Afrika zimejiunga katika ujenzi wa utaratibu huo.
Amesema kuwa utaratibu huo umetoa jukwaa kwa nchi za Afrika kushiriki katika mawasiliano ya kimataifa, na kwamba programu zake nyingi za mafunzo zimesaidia kuboresha uwezo wa kukusanya na kusimamia ushuru katika nchi husika za Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma