Lugha Nyingine
FOCAC lachangia utimiaji wa malengo ya maendeleo barani Afrika
Mkutano wa viongozi wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) wa mwaka 2024 utafanyika Beijing kuanzia tarehe 4 hadi 6 Septemba. Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania Prof. Humphrey Moshi amelipongeza Baraza hilo kwa mafanikio yake yaliyopatikana katika miaka zaidi ya 20 iliyopita tangu kuanzishwa kwake, na kusema Baraza hilo linachangia utimaji wa malengo ya maendeleo barani Afrika.
Akizungumza katika mahojiano na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG) yaliyofanyika hivi karibuni, Profesa Moshi amesema matokeo ya FOCAC yanahusisha sekta mbalimbali katika nchi za Afrika. Amesema kwa upande wa uchumi na biashara, China ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Afrika, na pia imewekeza kwa wingi katika sekta za miundo mbinu, madini, kilimo na viwanda, hivyo kusaidia katika ongezeko la uchumi wa nchi za Afrika ikiwemo Tanzania.
Pia amesema, ushirikiano kati ya Afrika na China umeisaidia Afrika kupunguza umaskini, kwani bara hilo lina nchi nyingi zinazoendelea, na kuwa na watu zaidi ya milioni 400 ambao wanaishi katika hali ya umaskini. Amesema kutokana na ushirikiano na China, viwango vya umaskini barani Afrika vinapungua. Aidha, chini ya mfumo wa FOCAC, China inaisaidia Afrika kuharakisha mchakato wake wa kuendeleza mambo ya viwanda.
Profesa Moshi amesema, uchumi wa Afrika hautegemei tu uzalishaji na uuzaji nje wa bidhaa na mazao ghafi, na kwamba mchakato wa maendeleo ya viwanda, ambavyo ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi na maendeleo unapata maendeleo kwa kasi.
Ameongeza kuwa, uzoefu wa China katika maendeleo ya viwanda umetoa mfano mzuri wa kuigwa kwa nchi za Afrika, na ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta ya viwanda unaharakisha mchakato huo wa maendeleo ya viwanda barani Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma