Lugha Nyingine
Wataalamu: Muunganisho na ushirikiano wa nishati ni muhimu kwa ujumuishi wa kifedha wa Afrika
Mhandisi akifunga kifaa cha usambazaji umeme kwenye kituo cha kuzalisha 400KV cha Konza katika Konza mji wa teknolojia wa Kenya. (Xie Songxin/China Daily)
Kuongezeka kwa zana za kifedha za kidijitali barani Afrika kupitia muunganisho wa simu za mkononi kumepanua upatikanaji wa huduma za kifedha, lakini kunazuiliwa na ukosefu wa upatikanaji wa nishati safi na yenye nafuu, walisema wataalamu waliokusanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, siku ya Jumatano, wakiongeza kuwa ushirikiano kati ya China na Afrika unaweza kusaidia kuziba pengo la upatikanaji wa nishati barani Afrika.
Akizungumza wakati wa Mkutano wa Ujumuishaji wa Kifedha wa Kidijitali wa China na Afrika 2024, Bei Duoguang, mkuu wa Chuo cha Ujumuishaji wa Kifedha cha China katika Chuo Kikuu cha Renmin cha China, alisema kwamba kipaumbele cha Afrika kinapaswa kuwa kufikisha maili ya mwisho kwa usambazaji wa nishati, ili kuwaleta watu wa maeneo ya mbali katika mifumo ya kifedha.
Bei alitoa mfano wa mfumo wa benki ya mtandaoni wa M-Pesa wa Kenya, ambao unaungwa mkono na jukwaa la huduma za kifedha la Huawei kama njia bunifu, kupitia njia hiyo Afrika inatumia teknolojia ya kidijitali kushughulikia huduma za kifedha. Hata hivyo, watu katika maeneo yasiyo na umeme wanapata changamoto za kutumia njia kama hizo, kwa sababu mambo rahisi kama kuchaji simu ni changamoto.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati, watu milioni 600 barani Afrika wanakosa umeme, alisema Bei. "Hata hivyo, Afrika ina uwezo mkubwa katika nishati mbadala kama vile ya jua, ambayo inaweza kusaidia wakulima na wafanyabiashara kupata nishati ya kuaminika," alisema.
Akirejelea Mkutano ujao wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), utakaofanyika Beijing mwezi ujao, Christine Mwangi, mratibu wa kikanda wa Shirika la Kuhifadhi Mazingira Duniani Afrika, alisema kwamba ahadi ya kuongeza biashara kati ya China na Afrika inaweza kufikiwa kupitia kilimo.
Changamoto bado ipo
Mwangi alisifu ushirikiano kati ya Afrika na China katika maeneo kama vile kukuza ongezeko la thamani na viwanda vya utengenezaji. Hata hivyo, nishati safi na zenye nafuu zinazohitajika kwa wakulima katika michakato kama vile kuongeza thamani au uzalishaji endelevu bado zinakabiliwa na changamoto.
Aliwataka watunga sera wa Afrika na China kuanzisha mifuko kupitia njia kama FOCAC kwa ajili ya kutoa nishati katika kilimo na uzalishaji, kwa kuwa kilimo endelevu ndiyo njia bora ya kulinda mazingira na kuhakikisha baioanuwai.
Ji Min, mkurugenzi wa Ofisi ya Mshauri katika Benki kuu ya China, alisema wanafanya kazi kusukuma mbele uwekezaji wa kijani, hasa katika biashara zinazohusika na nishati mbadala kama vile nishati ya upepo na ya jua kwa kampuni ndogo na za kati katika maeneo ya vijijini.
Mkutano huo wa siku moja uliwaleta pamoja washiriki zaidi ya 100, wakiwemo wataalamu kutoka sekta ya benki na ya kifedha, maafisa wa serikali pamoja na wataalamu kutoka taasisi za maendeleo na za biashara nchini China na Afrika.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma