Lugha Nyingine
Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda chaandaa mkutano wa mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Afrika
Profesa Buyinza Mukadasi akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano la kitaaluma kwa niaba ya naibu mkuu wa Chuo Kikuu cha Makerere katika Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala, Uganda, Agosti 12, 2024. (Picha na Hajarah Nalwadda/Xinhua)
KAMPALA - Wanataaluma kutoka Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda na taasisi kadhaa za China, kikiwemo Chuo Kikuu cha Xiangtan, wamekutana katika mji mkuu wa Uganda, Kampala siku ya Jumatatu na Jumanne kwa ajili ya kongamano linalolenga kuimarisha mawasiliano na maelewano ya utamaduni kati ya China na Afrika.
Buyinza Mukadasi, akizungumza kwa niaba ya makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Makerere, amebainisha kuwa kongamano hilo lililoanza siku ya Jumatatu na kuhitimishwa jana Jumanne linaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Makerere.
Ikiwa ilianzishwa kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Xiangtan na Chuo Kikuu cha Makerere Desemba 2014, taasisi hiyo imekuwa jukwaa muhimu la mawasiliano ya utamaduni, kuziba pengo kati ya China na Uganda na kuendeleza uraia wa kimataifa.
Kwenye kongamano hilo, wasomi wamejadiliana na kunufaishana utafiti kuhusu lugha, fasihi na mawasiliano ya utamaduni kati ya watu wa China na Afrika.
Pan Biling, mkuu wa Chuo Kikuu cha Xiangtan nchini China, alihutubia kongamano hilo kwa njia ya video, akisisitiza mchango mkubwa wa Xiangtan katika biashara, mawasiliano ya utamaduni, na ushirikiano wa kiufundi kati ya China na Afrika, na China na Uganda.
Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong amesema kuwa mawasiliano kati ya watu yamekuwa muhimu katika kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kwamba tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Confucius katika Chuo Kikuu cha Makerere, walimu wapatao 68 wa China wamekuja Uganda na kutoa mafunzo kwa Waganda zaidi ya 20,000 katika lugha ya Kichina na kwa walimu 177 wenyeji wa lugha hiyo ya Kichina.
"Madaraja yanajengwa ambayo yanaleta watu na mioyo yetu karibu," amesema Zhang, akibainisha kuwa ushirikiano katika elimu, afya, na mafunzo ya ufundi stadi umetoa matokeo yenye matunda. Pia ameeleza kuwa Pendekezo la Ustaarabu wa Dunia la China limepokelewa vyema na nchi za Afrika ikiwemo Uganda.
Kongamano hilo limeshirikiwa na maprofesa, madaktari, na wakuu wa vitivo kutoka Chuo Kikuu cha Nanjing cha China, Chuo Kikuu cha Ualimu cha Shanghai, Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, Chuo Kikuu cha Hohai na Chuo Kikuu cha Xiangtan.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma