Lugha Nyingine
Biden apimwa na kukutwa na maambukizi ya UVIKO-19: Ikulu ya White House
Rais wa Marekani Joe Biden akionekana pichani katika Ikulu ya Marekani White House mjini Washington, D.C., Marekani, Mei 13, 2024. (Picha na Aaron Schwartz/Xinhua)
WASHINGTON - Rais wa Marekani Joe Biden amepimwa na kukutwa na maambukizi ya UVIKO-19 siku Jumatano, Msemaji wa Ikulu ya Marekani White House Karine Jean-Pierre amethibitisha katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, akisema "Mapema leo kufuatia shughuli yake ya kwanza huko Las Vegas, Rais Biden amepimwa na kukutwa na UVIKO-19. Amechanjwa chanjo ya kwanza na za nyongeza, na ana dalili kidogo za kuugua,"
"Atarudi Delaware ambapo atajitenga kukutana na watu na ataendelea kutekeleza majukumu yake yote kikamilifu wakati huo," amesema.
"Rais ameonekana alasiri ya leo akiwa na dalili za tatizo la mfumo wa juu wa kupumua, ikiwa ni pamoja na rhinorhea (pua kutoa kamasi) na kikohozi kikavu, na kukosa utulivu kwa ujumla," kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa daktari wa Biden yaliyotolewa na Jean-Pierre.
Biden alikuwa amepangwa kuzungumza katika mkutano wa kikundi cha kutetea haki za kiraia cha Latino UnidosUS, lakini hataweza tena kuhudhuria.
"Kwa masikitiko, nilikuwa katika mawasiliano ya simu na Rais Biden na ameelezea masikitiko yake kwa kutoweza kuungana nasi mchana wa leo. Rais amekuwa kwenye hafla nyingi, kama tunavyojua sote, na amepimwa tu na kukutwa na UVIKO," Janet Murguia, mkuu wa kundi hilo, amewaambia waliohudhuria baada ya Biden kuchelewa kuonekana kwake.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Biden mwenye umri wa miaka 81 kukutwa na UVIKO-19. Hapo awali alipimwa na kukutwa na maambukizi hayo Mwaka 2022.
Habari hizi mpya zinakuja wakati Biden akikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa baadhi ya Wanachama wa Chama cha Democrat kujitoa kutoka kwenye kampeni za kugombea urais kutokana na wasiwasi kuhusu umri wake na utimamu wake wa kiakili kufuatia utendaji wake duni kwenye mdahalo dhidi ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mwishoni mwa Juni.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma