Lugha Nyingine
Uchumi wa China wadumisha upanuzi thabiti katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2024 licha ya changamoto
Picha hii ya droni iliyopigwa tarehe 20 Juni 2024 ikionyesha roboti zikifanya kazi kwenye karakana ya teknolojia za kisasa ya Kundi la Kampuni za Jiangsu Sanxiao katika Mji mdogo wa Hangji wa Mji wa Yangzhou, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China. (Xinhua/Li Bo)
BEIJING - Uchumi wa China umedumisha upanuzi thabiti katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2024 licha ya changamoto zinazoongezeka kutoka ndani na nje ya nchi hiyo, takwimu rasmi zilizotolewa Jumatatu zinaonesha ambapo pato la taifa (GDP) lilikua kwa asilimia 5 mwaka hadi mwaka kufikia yuan trilioni 61.68 (dola za Marekani takriban trilioni 8.65) na katika robo ya pili, Pato la Taifa la China liliongezeka kwa asilimia 4.7 mwaka hadi mwaka, Idara ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) imesema.
"Kwa ujumla, uchumi wa China umeendelea kuimarika katika nusu ya kwanza ya mwaka kwa njia tulivu," NBS imesema katika maoni yake mtandaoni, ikinukuu ni kutokana na motisha za sera, kurejea kwa nguvu kwa mahitaji ya nje na uendelezaji wa nguvu mpya za uzalishaji zenye sifa bora.
Mauzo ya rejareja nchini China yalipanda kwa asilimia 3.7 mwaka hadi mwaka katika nusu hiyo ya kwanza, wakati uwekezaji wa mali zisizohamishika ulipanda kwa asilimia 3.9 na pato la viwandani lililoongezwa thamani limeongezeka kwa asilimia 6.
Picha ya droni iliyopigwa tarehe 1 Aprili 2024 ikionyesha magari bidhaa yakisubiri kupakiwa kwa ajili ya kwenda kuuzwa nje ya nchi kwenye Eneo la Ghuba ya Zhifu katika Bandari ya Yantai, Mkoa wa Shangdong, Mashariki mwa China. (Xinhua/Li Ziheng)
Uhimilivu katikati ya changamoto
NBS imebaini ufanisi thabiti katika viashiria kadhaa muhimu. Kiwango cha ukosefu wa ajira mijini kilikuwa asilimia 5.1 katika nusu ya kwanza, ikishuka kwa asilimia 0.2 kutoka kipindi kama hicho mwaka jana.
Mapato ya kila mtu yanayotumika yalipanda kwa asilimia 5.4 mwaka hadi mwaka katika thamani halisi katika kipindi hicho, yakipita ukuaji wa uchumi.
Uzalishaji wa viwandani umegeuka kuwa wa kisasa na wa kijani, kwa mujibu wa NBS. Imesema, sekta ya viwanda vinavyotumia teknolojia ya hali ya juu iliongezeka kwa asilimia 8.7 mwaka hadi mwaka katika nusu ya kwanza, wakati uzalishaji wa roboti za huduma na magari yanayotumia nishati mpya umeongezeka kwa asilimia 22.8 na asilimia 34.3, mtawalia.
Mteja akinunua bidhaa kwenye supamaketi mjini Nanjing, Mkoa wa Jiangsu, Mashariki mwa China, Machi 9, 2024. (Picha na Liu Jianhua/Xinhua)
Misingi imara ya uchumi
NBS inatarajia hali ya kutokuwa na uhakika na ukosefu wa utulivu katika mazingira ya nje ya China kuendelea kuongezeka wakati changamoto za ndani ya China zikiendelea kuwepo katika nusu ya pili ya mwaka, lakini imesema ni "maumivu yanayoongezeka" na tiba iko katika maendeleo zaidi.
"Misingi ya uchumi ambayo itaendeleza ukuaji wa muda mrefu bado haijabadilika, na mwelekeo kuelekea maendeleo yenye ubora wa hali ya juu haujabadilika," NBS imesema, ikibainisha kuwa uchumi wa China bado ni injini kuu ya ukuaji duniani.
Taasisi nyingi za kigeni hivi karibuni zimeongeza makadirio yao ya ukuaji wa uchumi wa China. Barclays na Goldman Sachs zimeongeza makadirio yao ya ukuaji wa Pato la Taifa la China mwaka 2024 hadi asilimia 5 kutoka asilimia 4.4 na 4.8 mtawalia.
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) pia limerekebisha mtazamo wa uchumi wa China hadi asilimia 5, ikiwa ni pointi asilimia 0.4 zaidi ya makadirio ya awali.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma