Lugha Nyingine
Trump kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Chama cha Republican wiki hii licha ya kujeruhiwa kwenye mkutano wa hadhara
NEW YORK - Licha ya kujeruhiwa kwa kupigwa risasi kwenye mkutano wa hadhara wa Butler katika Jimbo la Pennsylvania nchini Marekani siku ya Jumamosi, timu ya kampeni ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump imesema atahudhuria Mkutano Mkuu wa Chama cha Republican unaoanza Jumatatu leo tarehe 15 (kwa saa za Marekani) kama ilivyopangwa ambapo katika taarifa ya pamoja, timu hiyo ya kampeni ya Trump na Kamati ya Taifa ya Chama cha Republican imesema rais huyo wa zamani "anaendelea vyema" na "anatarajia kuungana nanyi nyote huko Milwaukee tunapoendelea na mkutano mkuu wetu."
Mkutano Mkuu wa Chama cha Republican umepangwa kufanyika Milwaukee, Wisconsin, kuanzia leo Julai 15 hadi Julai 18, ambapo Trump anatarajiwa kuteuliwa rasmi kuwa mgombea wa rais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Novemba 5.
Risasi za moto zilifyatuliwa kwenye mkutano wa hadhara huko Butler, Pennsylvania Jumamosi jioni wakati Trump alipokuwa akitoa hotuba.
Mayowe yalisikika kutoka kwenye umati na Trump alionekana akiwa na damu kwenye upande wa kichwa chake na sikio lake, picha za video zinaonyesha. Haraka alisindikizwa ndani ya gari lake kabla ya msafara wake kuondoka mahali hapo.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema amepigwa risasi "iliyopenya sehemu ya juu ya sikio langu la kulia."
"Nilijua mara moja kuwa kuna kitu hakikuwa sawa katika hilo kwa kuwa nilisikia sauti ya kishindo, milio ya risasi, na mara moja nikahisi risasi imepasua kwenye ngozi," ameandika.
"Damu nyingi imetoka, kwa hivyo niligundua kile kinachotokea," akaongeza.
Trump amebainisha kuwa mtu mmoja ameuawa katika mkutano huo, na mwingine kujeruhiwa vibaya, akiongeza kuwa anatoa salamu za rambirambi kwa familia zao.
Kwenye taarifa yake kupitia mtandao wa X, Idara ya Siri ya Usalama ya Marekani imesema kwamba wakati wa mkutano wa Trump huko Butler, mtu anayeshukiwa kuwa mpiga risasi alifyatua "risasi nyingi" kuelekea jukwaani kutoka mahali pa juu nje ya ukumbi wa mkutano.
Maafisa wa Usalama "wamemdhibiti mpiga risasi, ambaye sasa ni marehemu," na rais wa zamani "yuko salama," imesema taarifa hiyo, ikiongeza kuwa mtazamaji mmoja wa mkutano huo ameuawa na wengine wawili wamejeruhiwa vibaya.
Rais wa Marekani Joe Biden amelaani shambulizi hilo siku ya Jumamosi.
"Hakuna mahali pa aina hii ya vurugu nchini Marekani. Ni lazima tuungane kama taifa moja ili kukemea," ameandika ujumbe kwenye mtandao wa X.
Katika hotuba yake iliyotolewa na Ikulu ya White House, Biden amesema amefahamishwa kwa kina juu ya tukio hilo.
Biden amezungumza na Trump kufuatia tukio hilo, kwa mujibu wa Ikulu ya White House.
"Hatuwezi kuruhusu tukio hilo kutokea. Hatuwezi kuwa hivi. Hatuwezi kupuuzia hili... Kila mtu lazima alaani," Biden amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma