Lugha Nyingine
Washiriki 124 kutoka nchi na maeneo 47 washindana kwenye Fainali za Kungfu za Michezo ya Shaolin
Wachezaji wa Kungfu wawili wakishindana kwenye Fainali za Michezo ya Shaolin 2024 katika Hekalu la Shaolin huko Dengfeng, Mkoa wa Henan wa China siku ya Jumapili. (Picha na Kan Li/CHINA NEWS SERVICE)
Fainali za Michezo ya Shaolin 2024 zimefikia tamati yake siku ya Jumapili, huku wale waliochukua nafasi 10 bora wakipata hadhi ya “Nyota wa Kung Fu ya Shaolin” baada ya mashindano ya siku mbili katika Hekalu la Shaolin lenye historia ndefu mkoani Henan, China.
Hekalu hilo la Shaolin ambalo limeandaa shughuli hiyo limesema, fainali hizo ni kilele cha mashindano ya mwaka mmoja ambao ulishuhudia wachezaji wa Kung Fu ya Shaolin zaidi ya 20,000 kutoka nchi na maeneo 101 wakichuania nafasi ya kushiriki fainali hizo. Kutoka kwenye washiriki hao wote, 2,400 walisonga mbele kwenye mashindano ya ngazi ya mabara, na hatimaye 124 walichomoza kutoka nchi na maeneo 47 kushindana kwenye fainali hizo pamoja na wataalamu wa Kung Fu ya Shaolin huko Dengfeng, Henan, China.
Watatu kati ya washindi hao kumi wanatoka China, wawili wanatoka Australia, na kulikuwa na mshindi kila mmoja kutoka Czech, Austria, Marekani, Peru na Zambia.
Korenc Karel, mshindi wa Czech mwenye umri wa miaka 18 amesema, kuingia kwenye nafasi 10 bora ni uthibitisho wa jitihada zake za miaka mingi katika kung fu.
“Nimekuwa nikifanya kung fu kwa miaka 12. Nilianza nilipokuwa na umri wa miaka 6, na ni kama nimekuwa nikifanya hivyo karibu maisha yangu yote,” amesema.
Ikiwa na historia ya zaidi ya miaka 1,500, Kung Fu ya Shaolin ni alama maarufu duniani kote ya utamaduni wa China, na iliorodheshwa kuwa urithi wa kitaifa wa utamaduni usioshikika mwaka 2006.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma