Lugha Nyingine
Kampuni ya China yafungua kiwanda cha kuzalisha vifaa visivyochafua mazigira vya kuezekea nyumba nchini Kenya
Wu Shuang (Wa kwanza kushoto, mbele), meneja mkuu wa Kampuni ya Vifaa vya Kuezekea Nyumba ya SINOMA, na Zhang Sicai (Wa kwanza kulia, mbele), meneja mkuu wa Kampuni ya Ujenzi ya CBMI wakimuonyesha bidhaa Wavinya Ndeti (Wa pili kushoto, mbele), Gavana wa Kaunti ya Machakos, katika Kaunti ya Machakos, Kenya, Juni 18, 2024. (Picha na Charles Onyango/Xinhua)
MACHAKOS, Kenya - Kampuni ya Kuzalisha Vifaa vya Kuezeka Nyumba ya SINOMA kutoka China imefungua kiwanda kipya nchini Kenya siku ya Jumanne ili kulipatia soko vifaa vya kuezekea nyumba ambavyo ni vya bei nafuu na vya kudumu zaidi visivyoleta uchafuzi kwa mazingira.
"Kenya na China zina uhusiano wa karibu wa urafiki. Tumedhamiria kutoa vifaa vya bei nafuu, vyenye sifa bora ambavyo vitakidhi mahitaji ya watu wa Kenya," amesema Wu Shuang, meneja mkuu wa kampuni hiyo, kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa kiwanda hicho ambacho kiko katika Kaunti ya Machakos, ambayo inapakana na mji mkuu Nairobi kwa upande wa magharibi.
“Tuna furaha kuwa teknolojia inayotumika itabadilisha namna uezekaji wa nyumba unavyofanywa, na kwamba kiwanda hiki kitatoa fursa kwa vijana kuja kujifunza jinsi teknolojia hii inavyofanya kazi,” amesema Wavinya Ndeti, Gavana wa Kaunti ya Machakos.
Ndeti ameelezea hamu yake kwa bidhaa za kiwanda hicho kipya, akisisitiza kuwa mambo ya uezekaji nyumba yanakabiliwa na ukuaji mkubwa na yana mahitaji makubwa.
Zhang Sicai, meneja mkuu wa Kampuni ya Ujenzi ya CBMI pia alishiriki kwenye shughuli za kuzinduliwa kwa kiwanda hicho.
Zhang amesema kiwanda hicho kitaajiri wafanyakazi wenyeji wasiopungua 50, huku kukiwa na mipango ya kuongeza idadi hiyo hadi kufikia 200 katika siku za baadaye.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo itafuata kwa makini matakwa ya usimamizi wa serikali ya Kenya ili kulinda mazingira, huku akirejelea hali isiyochafua mazingira ya vifaa hivyo vya kuezekea.
Maofisa husika wamesema kuanzishwa kwa kiwanda chenye ufanisi bora cha kuzalisha vifaa vya kuezekea nyumba kunakuja katika wakati muhimu ambapo Kenya inaendelea kutekeleza mpango kabambe wa nchi wa kutoa nyumba za bei nafuu katika miji na majiji ya nchi hiyo.?
Wafanyakazi wakiwa ndani ya kiwanda kipya kilichofunguliwa cha Kampuni ya Vifaa vya Kuezekea Nyumba ya SINOMA, katika Kaunti ya Machakos, Kenya, Juni 18, 2024. (Picha na Charles Onyango/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma