Lugha Nyingine
Mbinu za kilimo cha kisasa kinachozingatia tabianchi zawakinga wakulima wa Zimbabwe dhidi ya ukame
Marova Moyo, mkulima wa Zimbabwe, akionyesha ujuzi wa kilimo kwa wanakijiji wengine huko Mutoko, Jimbo la Mashonaland Mashariki, Zimbabwe, Juni 5, 2024. (Xinhua/Tafara Mugwara)
MUTOKO - Kwa fahari kubwa, Marova Moyo alikuwa akifurahia kuona maharage ya siagi ya kijani kwenye bustani yake huko Mutoko, wilaya iliyoko katika Jimbo la Mashonaland Mashariki la Zimbabwe. Kwa mkulima huyo mwenye umri wa miaka 62, hakuna kitu cha kumpa faraja kama kushuhudia mikunde ikistawi chini ya uangalizi wake.
Licha ya ukame unaosababishwa na El Nino unaoikabili Zimbabwe, Moyo na mumewe, Abel Katsande, bado wamevuna nafaka za kutosha kudumu hadi mavuno yajayo, kutokana na mbinu za kilimo cha kisasa zinazozingatia tabianchi ambazo zinahakikisha matumizi endelevu ya ardhi na rasilimali.
Baada ya kubaini kupungua kwa mavuno kutokana na kuzorota kwa ubora wa udongo, Moyo alianza kutumia kilimo hifadhi, mbinu ya kilimo cha kisasa ya tabianchi ambayo wakulima huchimba mashimo ili kuyatumia kama mabonde ambayo huhifadhi unyevu, kuwezesha mazao kustawi hata kwa maji machache.
"Tuligundua kuwa ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kwamba tunahifadhi udongo, kulinda afya zetu, na kulinda mazingira wakati huo huo kupata mavuno mengi," amesema Moyo katika mahojiano ya hivi majuzi na shirika la habari la China, Xinhua.
Dhana ya kilimo hifadhi inahusisha kiwango cha chini cha usumbufu wa udongo, kupanda mazao kwa mzunguko wa zamu, na matumizi ya matandazo. Matandazo husaidia kuhifadhi unyevu na kukandamiza magugu, wakati mbolea huboresha muundo wa udongo.
Moyo ni mwanachama wa Jukwaa la Wakulima Wadogo wa Zimbabwe (ZIMSOFF), shirika ambalo linajikita katika kuboresha maisha ya wakulima wadogo wanaofanya kilimo endelevu na cha kiikolojia.
Tangu alipoanza kutumia kilimo hifadhi kwenye kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari moja na nusu (kama hekta 0.61), mavuno yameongezeka zaidi ya mara mbili. Kitendo hicho pia kimemsaidia kufanya kilimo kuwa cha kibiashara.
Wakati mazao yanapovunwa, hakuna kitu kinachotupwa. "Kila kitu kinatumika hapa. Hata mashina ya mahindi tunayatumia kama matandazo, mengine kama chakula cha mifugo. Kinyesi cha mbuzi na kuku kinatumika kama samadi," Moyo amesema.
Kilimo cha kiikolojia kina mchango muhimu katika kuendeleza kilimo endelevu, amesema Patience Shumba, afisa wa programu ya ZIMSOFF.
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa mwezi Aprili alitangaza hali ya maafa kutokana na ukame uliosababishwa na El Nino ambao uliyafanya mahindi katika maeneo mengi ya nchi hiyo kuwa yasiyoweza kuzaa matunda.
Watu takriban milioni 9, zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote nchini humo, watahitaji msaada wa chakula hadi kufikia Machi mwaka ujao, kwa mujibu wa serikali.?
Marova Moyo, mkulima wa Zimbabwe, akiweka matandazo ya kulinda mimea kwenye zao la maharage ya siagi huko Mutoko, Jimbo la Mashonaland Mashariki, Zimbabwe, Juni 5, 2024. (Xinhua/Tafara Mugwara)
Kahukwa Kanyonganise, mkulima wa Zimbabwe, akionekana kwenye shamba lake la pilipili hoho huko Mutoko, Jimbo la Mashonaland Mashariki, Zimbabwe, Juni 5, 2024. (Xinhua/Tafara Mugwara)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma