Lugha Nyingine
Rais Xi Jinping atoa salamu za rambirambi kwa?kifo cha Rais wa Iran
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping ametoa salamu za rambirambi kwa kifo cha Rais wa Iran Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin amesema siku ya Jumatatu. Katika salamu zake hizo zilizotumwa kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Mokhber, Rais Xi akiwa kwa niaba ya serikali ya China na watu wa China, ametoa salamu za rambirambi na pole za dhati kwa Mokhber, familia ya Rais Raisi, serikali ya Iran na watu wa nchi hiyo.
Rais Xi amesema, tangu Rais Raisi aingie madarakani, ametoa mchango muhimu katika kudumisha usalama na utulivu wa Iran na kuhimiza maendeleo na ustawi wa nchi. Ameongeza kuwa Raisi pia amefanya juhudi za kuimarisha na kuzidisha ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Iran.
“Kifo cha kusikitisha cha Raisi ni hasara kubwa kwa watu wa Iran, na watu wa China pia wamepoteza rafiki mzuri,” Rais Xi amesema.
Serikali ya China na watu wa China wanathamini urafiki wa jadi kati ya China na Iran, Rais Xi amesema, akisisitiza kuwa kwa juhudi za pamoja za pande zote mbili, ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Iran utaendelea kuimarika na kustawi.
“China pia imetuma salamu za dhati za rambirambi kwa kifo cha kusikitisha cha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na kutoa salamu za rambirambi kwa familia yake,” Wang ameongeza.
Msemaji huyo amesema, baada ya ajali hiyo, China ilifuatilia kwa karibu sana na kueleza nia yake ya kutoa uungaji mkono na msaada unaohitajika kwa Iran.
Wang amesema China itaendelea kuunga mkono serikali ya Iran na watu wa nchi hiyo katika kudumisha hali ya kujiamulia mambo yao kwa uhuru, utulivu na maendeleo, na ingependa kushirikiana na Iran katika kuzidisha zaidi ushirikiano wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Iran.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma