Lugha Nyingine
Kenya yatoa wito kwa viongozi wa Afrika kuweka mikakati ya kufanya mbolea iwe nafuu
Rais wa Kenya William Ruto Alhamisi alitoa wito kwa viongozi wa Afrika kuweka mikakati ya kufanya mbolea iwe rahisi na iwafikie wakulima.
Ruto, ambaye alifungua Mkutano wa Kilele wa Mbolea na Afya ya Udongo barani Afrika, mjini Nairobi, Kenya, alisisitiza haja ya ushirikiano kati ya nchi za Afrika ili kuongeza uwezo wa bara la Afrika kuzalisha mbolea kwa kutumia malighafi zinazopatikana ndani.
Zaidi ya wajumbe 2,000 wakiwemo mawaziri, watafiti, wafadhili na marais sita wa Afrika wanahudhuria mkutano huo wa siku tatu. Ukiwa umeandaliwa pamoja na Umoja wa Afrika, serikali ya Kenya, na washirika wa kimataifa, mkutano huo wenye kaulimbiu "Sikiliza Ardhi," unatarajiwa kuandaa njia mpya ya kuzalisha upya udongo wa bara hilo na mifumo mingine muhimu ya ikolojia.
Wakati huohuo, kwenye tamko lao la pamoja, wakuu wa nchi na serikali za Afrika wamepitisha mpango wa utekelezaji wa kina ili kurejesha afya ya udongo kupitia kuongeza matumizi ya mbolea katika uzalishaji wa chakula. Viongozi hao wameazimia kuongeza tija ya ardhi kwa kilimo kupitia matumizi ya mboji na samadi. Wameapa kuongeza mara tatu uzalishaji wa ndani na usambazaji wa mbolea ya kikaboni na isiyo ya kaboni iliyoidhinishwa ifikapo mwaka 2034 ili kuboresha upatikanaji na bei nafuu kwa wakulima wadogo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma